Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi ya korosho yapewa maagizo kusimamia pembejeo

Koroshoooooo Bodi ya korosho yapewa maagizo kusimamia pembejeo

Mon, 22 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ameitaka Bodi ya Korosho nchini kufanyia kazi changamoto zilizopo ili kuhakikisha usambazaji wa pembejeo za kilimo cha korosho zinatekelezwa kwa wakati.

Ndemanga amebainisha hayo leo Aprili 21, 2024 katika kijiji cha Kiwalala kilichopo Wilaya ya Lindi mkoani humo, wakati wa uzinduzi wa shughuli ya ugawaji wa pembejeo na mfumo mpya wa Tehama ambao unatumika nchi nzima.

Mkuu huyo wa wilaya amesema ugawaji wa pembejeo kwa wakulima lazima uzingatie changamoto mbalimbali ikiwemo udanganyifu.

Amesema Bodi ya Korosho ihakikishe pembejeo zinafika kwa walengwa kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na hali mbaya ya miundombinu ya barabara, zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani hapa.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary amewataka wakulima wa korosho kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wanasajiliwa kwenye mfumo wa Tehama ambao utatumika katika shughuli ugawaji wa pembejeo.

Amesisitiza kuwa wananchi waache imani potofu kwenye suala la usajili linaloendelea na badala yake wajitokeze, ili wanufaike na pembejeo kama ilivyokuwa msimu uliopita wa mwaka 2023/2024.

Ameiomba Bodi ya Korosho kuzingatia changamoto za wakulima zinazowakabili kutokana na mazingira na hali ya hewa, ili kuhakikisha hakuna mkulima hata mmoja anakosa pembejeo.

Mkurugenzi wa bodi hiyo, Francis Alfred akitoa taarifa ya maandalizi ya msimu wa kilimo cha korosho kwa mwaka 2024/2025, amesema Serikali imeweka malengo ya kuongeza uzalishaji kwa mti wa korosho kutoka kilogramu 10 mpaka 30 ili iweze kuzalisha tani 700,000 hadi kufikia 2025/26.

“Kwa msimu wa kilimo 2024/25, Serikali imepanga kuongeza uzalishaji wa zao la korosho kutoka tani 305,000 mpaka tani 595,000 ambapo imejipanga kuwapatia wakulima pembejeo za ruzuku kiasi cha tani 30,000 za sulphur na viuatilifu vya maji lita 3,800,000."amesema Alfred.

Hata hivyo, mkulima wa Kijiji cha Mtua kilichopo katika Halmashauri ya Mtama, Seifu Bakari ameishukuru Serikali pamoja na bodi kwa kuwaletea pembejeo mapema, tofauti na miaka mingine zilikuwa zinachelewa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live