Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT yazungumzia mwongozo wa usajili vikundi vya fedha

A5cbb8f4b667df3a8d40f559b76bee5a.png BoT yazungumzia mwongozo wa usajili vikundi vya fedha

Thu, 4 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema imeshaandaa mwongozo na mfumo wa kielektroniki wa usajili wa vikundi vya huduma za fedha.

Imesema lengo ni kudhibiti baadhi ya watu ambao walikuwa wanatoa mikopo ya fedha pasipo kuzingatia taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yameelezwa jijini hapa na Mkurugenzi kutoka BoT( Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Jerry Sabi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa maofisa maendeleo ya jamii kuhusu utekelezaji wa mfumo na mwongozo wa usajili wa vikundi vya kijamii katika sekta ya fedha nchini.

Alisema lengo la kuanzishwa kwa mfumo huo ni kuwa sekta ya fedha imekuwa na watu ambao mwenendo wao wa biashara ya fedha sio mzuri na mtu anaweza kukopa fedha kutoka benki au taasisi ya fedha bila kurejesha.

Alisema mwaka 2018 Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, ambayo pamoja na mambo mengine, imeipa Benki Kuu ya Tanzania jukumu la usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha kwa Tanzania Bara ambao wamegawanya katika madaraja manne.

Watoa huduma hao ni benki zinazochukua amana za umma, wasiopokea amana za umma ikijumuisha kampuni na watu binafsi wanaotoa mikopo na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ikiwemo Vicoba.

Alisema serikali kwa kutambua ukubwa wa majukumu hayo ya kisheria, Kifungu cha 14 cha Sheria ya Huduma za Fedha ya Mwaka 2018, Novemba 13 mwaka 2019 kiliipa BoT uwezo wa kukasimisha mamlaka na majukumu yake kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Serikali za Mitaa, ambapo Benki Kuu kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Ofisi ya Rais Tamisemi katika kufanya maandalizi ya usajili na usimamizi wa watoa huduma za fedha nchini.

Alisema mwongozo na mfumo huo unalenga kuwawezesha watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusajili vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kwa mujibu wa Kanuni ya 8 ya kanuni za huduma ndogo za fedha za mwaka 2019.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu-Tamisemi, Antelma Mtemahanji alisema Tamisemi imekasimiwa majukumu ya kusimamia vikundi vyote ambavyo vilikuwa vikifanya biashara ya fedha bila kujisajili, ambavyo kwa sasa lazima visajiliwe kwa mujibu wa sheria.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk Emmanuel Kipore ameishukuru BoT kwa utoaji wa mafunzo hayo kwa watendaji hao ambayo yataleta tija kwa wananchi hususani wale ambao wamekuwa wanakwenda kuomba mikopo kwenye taasisi za fedha na kukabiliwa na changamoto.

Chanzo: www.habarileo.co.tz