Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT yazipa mbinu benki kupunguza riba

07bb2640566bbfd2789cf9af9426fad5 BoT yazipa mbinu benki kupunguza riba

Wed, 23 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Dk Bernard Kibese ameagiza taasisi za fedha na benki zote nchini, kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji ili kumudu kupunguza riba kwa wateja wao.

Alisema hayo wakati wa uzinduzi wa huduma ya malipo, inayotumia mfumo wa kadi ya viza kutoka Benki ya Letshego Dar es Salaam jana.

Kibese alisema ni muhimu kuwezesha kupunguza gharama za riba katika mikopo na huduma nyinginezo, ili miaka mitano ijayo Tanzania ifikie katika hatua ya uchumi ya tarakimu moja.

“Benki zote hapa nchini zihakikishe zinapunguza kwa kiasi kikubwa mikopo isiyolipika, ziwe na mitaji mikubwa, ziwe tayari kuongeza na kuanzisha huduma zenye ghrama nafuu, lakini pia benki hizi ziwezeshe kupunguza gharama za riba katika mikopo yao na huduma zingine ili ndani ya miaka mitano tuweze kufikia hatua ya kiuchumi ya tarakimu moja,” alisema Dk Kibese.

Aliongeza kuwa riba kubwa, huathiri wananchi na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi, hivyo taasisi za fedha ziwekeze katika tafiti ili kuweza kubuni miradi mipya ya uendeshaji taasisi zao.

“Taasisi za fedha ziwekeze sasa katika tafiti ili kuweza kuvumbua huduma mpya hususani za kidigitali zitakazoendana na teknolojia, huduma hizi zihakikishe usalama wa wateja wenu na wananchi kwa ujumla,”alisema.

Aliipongeza Benki ya Letshego kwa kuanzisha huduma ya malipo kwa mfumo wa kadi ya viza. Alieleza kuwa elimu ya matumizi ya kidijitali katika mifumo ya malipo ni muhimu ikazingatiwa, kwani teknolojia inakua kwa kasi na watu wana haki ya kupata elimu ya matumizi mapya ya huduma za kifedha.

“Nawapongeza Letshego kwa maendeleo haya makubwa kwenu na sekta ya uchumi nchini, naendelea kuwasisitiza mtoe elimu na chachu ili watu waweze kutumia huduma hizi mpya za kifedha kwa ufasaha zaidi bila usumbufu, hii iende kwa taasisi zote za fedha na benki nchini,”aliongeza.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Benki ya Letshego, Andrew Tarimo alisema uzinduzi wa huduma hii ni mwendelezo wa uvumbuzi wa matumizi ya teknolojia katika mifumo ya utoaji huduma za Benki ya Letshego.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Letshego, Noel Sangiwa, alisema wateja wa benki hiyo waendelee kuwa wavumilivu, kwani mabadiliko ya kiteknolojia yatakuwa mengi katika taasisi hiyo, ambayo bado inapanua wigo wa huduma zake za kifedha.

Chanzo: habarileo.co.tz