Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT yawatuliza wateja wa benki 7

1e9316f16c4b7699174f9b0d3efb0a87 BoT yawatuliza wateja wa benki 7

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Fedha na Mipango imewahakikishia wateja wenye amana katika benki saba zilizofutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuwa utaratibu wa ukusanyaji mali na madeni unaendelea kufanywa na Bodi ya Bima ya Amana (DIB). Wateja hao ni wale wenye amana za zaidi ya Sh milioni 1.5.

Katika mwaka wa fedha 2017/18, BoT ilizifutia leseni ya kufanya biashara ya kibenki Benki ya FBME, Benki ya Wananchi Mbinga, Njombe, Meru, Benki ya Wakulima Kagera, Efatha na Benki ya Wanawake Covenant.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis, bungeni jijini Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Jang’ombe , Ali Hassan King (CCM).

Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua serikali imefikia hatua gani katika kufuatilia fedha za wananchi zilizopo katika benki zilizozuiliwa kuendesha shughuli zao hapa nchini.

Akijibu swali hilo, naibu waziri alisema baada ya kuzifutia leseni benki hizo saba, BoT iliiteua DIB kuwa mfilisi.

Alifafanua kuwa katika kutimiza wajibu wake wa msingi wa kisheria, DIB ilianza kulipa fidia ya Bima ya Amana ya hadi Sh milioni 1.5 kwa waliostahili kulipwa katika benki hizo na zoezi hilo bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia.

Aidha, alisema DIB inaendelea na ufilisi wa benki hizo ambapo hadi kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka jana Sh bilioni 4.9 zimelipwa kwa wateja wenye amana wa benki sita za wananchi isipokuwa Benki ya FBME.

Alieleza kuwa malipo hayo ni sawa na asilimia 77.27 ya kiasi cha Sh bilioni 6.3 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia.

Alisema pia jumla ya wateja waliolipwa ni 21,675 kati ya wateja 57,076 ikiwa ni asilimia 37.98 ya wateja waliokuwa na amana zilizostahili fidia.

Akielezea upande wa benki ya FBME, alifafanua kuwa hadi mwishoni mwa Desemba mwaka jana, kiasi cha Sh bilioni 2.4 zimelipwa kwa wateja wenye amana ambazo ni sawa na asilimia 52.13 ya kiasi cha Sh bilioni 4.6 kilichotengwa.

Alisema jumla ya wateja waliolipwa ni 3,443 kati ya wateja 6,628, ambao ni sawa na asilimia 51.95 ya wateja waliokuwa na amana zilizostahili fidia.

Alieleza kuwa wateja waliokuwa na amana inayozidi Sh milioni 1.5, watalipwa kiasi kilichobakia chini ya ufilisi, ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi, kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za benki husika.

Chanzo: habarileo.co.tz