Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT yawashushia rungu wanaokopesha bila leseni

Hii Hapa Tamko La Kamati Ya Fedha Kutoka BOT BoT yawashushia rungu wanaokopesha bila leseni

Sat, 6 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati kukiwa na changamoto ya mikopo umiza nchini, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema ni kosa kwa taasisi, kampuni au mtu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila leseni.

 Katazo hilo limetajwa kuwa ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 16 kifungu cha kwanza (1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, Januari 5, 2024 na Gavana wa BOT , Emmanuel Tutuba imesema haitasita kuwachukuliwa hatua za kisheria wale wote wanaofanya biashara hiyo kinyume cha sheria.

Aidha kwa mujibu wa kifungu cha 16(2) (a) cha sheria hiyo hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukwaji wa sheria ni faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo kisichopungua miaka miwili au vyote kwa pamoja.

“Benki Kuu inawakumbusha wakopaji wote kuhakikisha wanasoma mikataba ya mikopo inayotolewa na wakopeshaji, kuelewa na kukubaliana na vigezo na masharti ikiwa ni pamoja na riba na gharama nyingine za mikopo hiyo,” amesema na kuongeza;

“Tunasisitiza mkopeshaji anatakiwa kutoa nakala ya mkataba wa mkopo kwa mkopaji, kadhalika mkopaji ana haki ya kudai na kupewa mkataba wa mkopo kila anapochukua mkopo.”

Tutuba ameusisitizia umma kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye hana leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Amesema orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zinatolewa na BoT kwenye tovuti yake kupitia kurugenzi ya usimamizi wa sekta ya fedha, idara ya usimamizi wa taasisi za huduma ndogo za fedha Benki Kuu ya Tanzania.

Wakati BoT wakitoa agizo hilo, Agosti 16, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiwa Kinondoni aliagiza kukamatwa wakopeshaji wanaofanya hiyo shughuli kinyume cha taratibu.

Pia, Agosti 19 , 2023 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga aliwataka walimu kuachana na mikopo umiza na kausha damu na badala yake wakope kwenye taasisi rasmi za fedha ikiwemo benki.

Hata hivyo, Julai 2023 Tutuba aliwataka Watanzania kuwa makini na taasisi ndogo za ukopeshaji alizosema zimegawanyika katika makundi matatu, za ngazi ya jamii (vikoba), Saccos na kampuni au mtu binafsi ambazo haziruhusiwi kukusanya dhamana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live