Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezionya taasisi na watu binafsi wanaotoa huduma za mikopo bila kusajiliwa na kutoza riba kuliko kiwango kilichowekwa cha asilimia 3.5 kwa mwezi.
Katika ufunguzi wa semina ya siku moja kwa wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa BoT na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kufanyika Dar es Salaam, Naibu Gavana wa BoT, Julian Banzi alisema katika jamii kumekuwa na kilio kuhusu kuwepo ‘mikopo umiza’.
Maofisa wa BoT walisema hakuna sheria ya mikopo midogo kwa wananchi wanyonge inayoruhusu riba ya mkopo kuvuka asilimia 3.5 kwa mwezi na kwamba hicho ndicho kiwango cha kisheria cha riba kwa mikopo ya watu hao.
Mchambuzi Mkuu wa Biashara wa BoT, Mary Ngassa, alisema: “Miongoni mwa vipengele tunavyopitia wakati wa kusajili taasisi au watu binafsi wanaotoa huduma ndogo za kifedha ni pamoja na kiwango cha riba ambayo ni asilimia 3.5 kwa mwezi au asilimia 42 kwa mwaka.”
“Hakuna sera ya mikopo midogo yenye riba zaidi ya asilimia 3.5, hivyo kutoza riba zaidi ya hapo, ni kosa kubwa na tunaomba mtujulishe watu hao maana hata wanaokopesha bila leseni ni wahalifu.