Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imepandisha Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.5 iliyotumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 hadi asilimia sita, ambayo itatumika katika robo ya pili ya mwaka 2024, huku ikielezea mwenendo wa thamani ya Shilingi.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa benki na waandishi wa habari, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema uamuzi wa kuongeza riba ulifikiwa katika kikao cha kamati kilichofanyika jana Aprili 3, 2024 na umezingatia tathimini ya mwelekeo wa uchumi iliyofanyika Machi 2024.
Gavana Tutuba amesema lengo ni kudhibiti mfumko wa bei nchini ambao kwa sasa upo wastani wa asilimia tatu.
“Kamati imeona umuhimu wa kuongeza riba ya Benki Kuu hadi asilimia sita, itakayokuwa na wigo wa asilimia mbili juu na chini, ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei siku zijazo kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa dunia,” amesema.
Amesema benki zenye ukwasi mdogo zitapata fedha hadi kwa asilimia nne.
Gavana Tutuba amesema katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sambamba na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha na bei za bidhaa katika soko la dunia imebaki tulivu.
“Mathalani, bei ya mafuta ghafi ilikuwa wastani wa Dola 80 za Marekani kwa pipa, wakati bei ya dhahabu imeendelea kubaki juu, ikiuzwa kwa wastani wa Dola 2,071 kwa wakia moja. Hali hii inatarajiwa kuendelea katika kipindi kijacho cha mwaka 2024,” amesema.
Hata hivyo, amesema matarajio hayo yanaweza kuathiriwa na uamuzi wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi (OPEC+) kuhusu kiwango cha uzalishaji na migogoro ya kisiasa inayoendelea.
Gavana Tutuba amesema akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha, kufikia zaidi ya Dola 5.3 bilioni mwishoni mwa Machi 2024, sawa na miezi 4.4 ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.
Amesema nakisi ya urari wa biashara nje ya nchi iliendelea kupungua kutokana na kupungua kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi.
Katika mwaka unaoishia Februari 2024, nakisi ilipungua kufikia Dola milioni 2,701.4 kutoka Dola milioni 5,133.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Kuhusu thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani, amesema ilipungua kwa asilimia 1.8 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 1.6 katika robo ya mwisho ya mwaka 2023.
“Hali hii ilitokana na msimu wa mapato madogo ya fedha za kigeni na mazingira ya kiuchumi duniani. Kamati pia ilijadili kuhusu changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni nchini na kujiridhisha kwamba, hatua za kuongeza upatikanaji na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotekelezwa hivi sasa zinatarajiwa kupunguza changamoto hiyo ndani ya muda mfupi ujao,” amesema.
Kuhusu hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi ameishukuru BoT kwa usimamizi wa sekta ya fedha nchini, akiomba suala la uhaba wa Dola liendelee kushughulikiwa.
“Taarifa ya uamuzi wa riba imetolea vizuri, lakini kuendelea kufanyia kazi suala la uhaba wa fedha za kigeni ni jambo la muhimu. sera ya fedha inasimamiwa vizuri tutakuwa na maoni katika majukwaa yetu mengine,” amesema Sabi.