Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT yapunguza riba tena, wakopaji wachekelea

13916 BOT+PIC TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wananchi wa kawaida na wafanyakazi watapata ahueni ya kukopa katika benki mbalimbali nchini huku riba zikitarajiwa kupunguzwa tena na muda wa kurudisha mikopo kuongezwa.

Ni dhahiri kuwa sasa wafanyabiashara wadogo, wananchi wa kawaida, wafanyakazi na sekta binafsi za biashara zitapata fursa ya kukopa na sifa ya kukopesheka baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT)kupunguza riba kwa benki nchini kutoka asilimia tisa hadi saba.

Punguzo hilo la riba linazipa benki fursa ya kukopa na kurudisha kwa riba ndogo zaidi.

Suala hilo linaweza kusababisha mwananchi wa kawaida kuwa na sifa ya kukopesheka katika benki, kurudisha kwa muda mrefu kwa riba ndogo.

Punguzo hilo la riba litaanza rasmi Agosti 27 na litaendelea hadi yatakapofanyika mapitio mapya.

Barua ya Naibu Gavana wa BoT anayesimamia sera za uchumi na fedha (EFP), Dk Yamungu Kayandabila iliyoandikwa Agosti 23 kwenda kwa benki za biashara na taasisi za fedha inabainisha kushuka kwa riba hiyo kwa asilimia mbili huku utekelezaji wake ukielezwa kuanza kesho.

“Kama nilivyowaeleza kwenye waraka wa Agosti 3, 2017, nawafahamisha kupungua kwa riba itakayotozwa kwenye mikopo yote ambayo benki za biashara zitakopa kutoka Benki Kuu pamoja na amana za Serikali mpaka asilimia saba kutoka asilimia tisa iliyokuwapo (na) itakayotumika mpaka marekebisho mengine yatakapofanyika,” inasomeka taarifa hiyo. Nakala ya barua hiyo pia imepelekwa kwa katibu mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.

Nakala nyingine imekwenda kwa Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Uamuzi huo unakusudia kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wananchi na sekta binafsi ili kufanikisha sera ya uchumi wa viwanda inayopewa kipaumbele na Serikali.

Katika taarifa hiyo, Dk Kayandabila alisema mabadiliko hayo yamezingatia mwenendo wa mauzo ya hatifungani za Serikali hasa zinazoiva baada ya siku 91 au 182.

“Mapitio haya yanadhihirisha juhudi za makusudi kukuza kiasi cha mikopo inayotolewa kufanikisha shughuli za uchumi,” ameandika Naibu Gavana kwenye taarifa yake kwa umma.

Akizungumzia punguzo hilo, mhadhiri mwandamizi na mtaalamu wa masuala ya uhasibu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Ernest Kitindi alisema kupungua kwa gharama za kukopa ni suala jema ambalo kwa muda mrefu ujao litakuwa na mchango chanya kwenye uchumi endapo litakuwa endelevu.

“Awali riba ilikuwa imeachana sana na mahitaji. Uwezo wa wakopaji ulikuwa mdogo kuliko riba iliyokuwa inatozwa. Kinachofanyika sasa ni kujaribu kuzikutanisha nguvu za soko. Riba inawafuata wateja. Kumbuka, mtu anaweza akaahirisha kununua bidhaa au huduma aitakayo kama bei yake ni ghali,” alisema Profesa Kitindi.

Ndani ya mwaka mmoja na nusu, BoT imeshuka kwa zaidi ya nusu riba ya mikopo hivyo kuzishawishi benki za biashara nazo kufanya hivyo na kuwapa unafuu wananchi wachache wanaonufaika moja kwa moja na sekta ya fedha nchini.

Machi mwaka jana, BoT ilishusha riba kwa asilimia nne kutoka asilimia 16 mpaka asilimia 12. Agosti mwaka huo huo ikashusha tena mpaka asilimia tisa iliyodumu mpaka sasa.

Kutokana na mabadiliko hayo ya gharama za ukopaji, benki nyingi za biashara zimeshusha riba ya mikopo inayotoa huku zikiongeza muda wa marejesho ili kuwaruhusu wananchi kukopa kiasi kikubwa zaidi kwa makato madogo tofauti na ilivyokuwa zamani.

Mwaka mmoja tangu ilipofanya mabadiliko hayo, kuanzia kesho wadau wa sekta binafsi wataanza kushuhudia unafuu mwingine sokoni. Hata hivyo, takwimu zinaonyesha ni takriban asilimia 17 tu ya Watanzania wote wanatumia huduma za fedha.

Lakini licha ya kushuka kwa riba kwa kipindi hicho, ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya hali ya uchumi mwaka 2017 inaonyesha kushuka kwa kiwango cha mikopo ya nyumba kwa asilimia 17 na kufika Sh344 bilioni licha ya upungufu wa nyumba milioni tatu uliopo nchini.

Profesa Kitindi alisema kushushwa kwa riba ni suala moja na mwitikio wa wateja ni suala jingine. “Baada ya riba kushuka tunahitaji kuona soko (litaitikia) lita-respond vipi. Riba inaweza ikashuka lakini uchumi usikue kwa matarajio yaliyokuwepo hivyo mchango wake kutoonekana haraka,” alisema.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Omari Mbura alisema benki za biashara nazo zikipunguza zaidi riba zao kwa mikopo inayotolewa, shughuli nyingi za uchumi zitachangamka kwani hata wafanyabiashara wadogo watakuwa na sifa za kukopesheka.

Alisema zamani riba ilipokuwa juu iliwalazimu wajasiriamali kufikiria aina za biashara zenye faida kubwa ili kuweza kurejesha mikopo husika ndani ya muda uliotolewa hali ambayo kwa sasa itabadilika.

Si hivyo tu, alisema suala hilo pia litachochea ujasiriamali kwani litawakatisha tamaa waliokuwa wanaweka fedha kwenye akaunti za muda maalumu lakini kwa punguzo hili watalazimika kutafuta vyanzo vingine vya uwekezaji. “Ni wakati muafaka kwa (taasisi ndogo za fedha) microfinance zitakua zaidi kwa kuwavutia wawekezaji hawa. Vilevile wenye mitaji wataanza kufikiria miradi ambayo (faida) return yake inazidi riba ya benki. Hii itahamasisha ujasiriamali,” alisema Dk Mbura.

Chanzo: mwananchi.co.tz