Dar es Salaam. Kutokana na mwenendo usioridhisha wa Benki ya TIB Corporate, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesitisha uteuzi wa, Frank Nyabundege aliyekuwa mkurugenzi mtendaji kuanzia Julai 13, 2019.
BoT imetumia mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 kusimamisha ukurugenzi wa Nyaundege aliyeiongoza benki hiyo tangu Agosti Mosi, 2014.
“Hatua hizi zina lengo la kuboresha usimamizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali. Benki Kuu ya Tanzania inauhakikishia umma kuwa Benki ya TIB Corporate itaendelea kutoa huduma na madai yote yaliyoiva yatalipwa kama kawaida,” inasomeka sehemu ya taarifa iliyotolewa na BoT.
BoT imeeleza kuwa imechukua uamuzi huo kutokana na mwenendo usioridhisha wa TIB Corporate na imemteua Fred Luvanda kutoka kurugenzi yake ya usimamizi wa sekta ya fedha kuwa kaimu mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo.
BoT imesema itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika benki kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa stahimilivu na kuchangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kuondolewa kwa Nyabundege kumefanywa baada ya BoT kuzifunga benki kadhaa ndani ya miaka minne iliyopita katika maeneo tofauti nchini huku baadhi zikilazimishwa kutafuta wabia wa kuungana nao kutokana na mwenendo usiridhisha.
Pia Soma
- Alichokisema Mtatiro baada ya kuteuliwa kuwa DC Tunduru
- MAHIUBIRI YA JUMAPILI: Fahamu jinsi ya kuponya katika maisha ya mwanadamu
- Ukosefu wa fedha, chanzo cha upungufu wa nguvu za kiume
BoT inadhamana la kumthibitisha mtu yeyote anayependekezwa na bodi ya wakurugenzi kuwa mkurugenzi mtendaji wa benki au taasisi yoyote ya fedha nchini.