Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT yaeleza sababu kuimarika uchumi

Bot Two BoT yaeleza sababu kuimarika uchumi

Thu, 25 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeridhishwa na kasi ya ukuaji uchumi nchini unaotarajiwa kukua kwa asilimia 5.2 mwaka huu.

Taarifa ya BoT imeeleza kuwa mwendendo wa ukuaji wa uchumi nchini umeendelea kuwa wa kuridhisha kutokana na kuimarika kwa mazingira ya kibiashara, uwekezaji unaoendelea kufanywa na sekta ya umma na binafsi, kuimarika kwa shughuli za utalii na ongezeko la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

BoT ilieleza kuwa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi kwenye uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei wakati ikichangia ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta ya fedha.

“Utekelezaji huo uliwezesha ongezeko la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, na kusaidia kuweka mazingira mazuri ya kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini,” ilieleza BoT.

BoT ilieleza kuwa utekelezaji wa sera ya fedha ulisaidia kufikiwa malengo yaliyoainishwa kwenye Programu ya ‘Extended Credit Facility (ECF)’ Machi mwaka huu na kuweka msingi thabiti wa kufikiwa malengo ya programu hiyo Juni mwaka huu.

Taarifa ilieleza kuwa ukuaji wa uchumi katika robo tatu za mwaka jana Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 5.2 na unatarajiwa kukua kwa takriban asilimia tano mwaka mzima wa 2022 na asilimia 5.2 kwa mwaka huu.

“Kwa upande wa Zanzibar, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2022, ukiwa juu ya ukuaji wa asilimia 5.1 kwa mwaka 2021. Uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.1 kwa mwaka 2023, sambamba na jitihada zinazoendelea za kuimarisha uchumi wa bluu, sera nzuri za kiuchumi na kuendelea kuimarika kwa shughuli za utalii,” ilieleza taarifa ya BoT.

BoT ilieleza kuwa mapato ya ndani yalifikia asilimia 95.1 ya lengo kwa Tanzania Bara, na asilimia 95.9 ya lengo kwa upande wa Zanzibar.

Taarifa ilieleza kuwa hiyo ni dalili ya kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi sanjari na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato na utayari wa walipa kodi katika kulipa kodi kwa wakati.

BoT ilieleza kuwa matumizi ya serikali yameendelea kufanyika kulingana na rasilimali fedha zilizopo katika kukidhi vipaumbele vilivyowekwa ndani ya bajeti ya mwaka 2022/23.

Taarifa ilieleza kuwa sekta ya kibenki iliendelea kuwa imara na thabiti yenye kiwango cha kutosha cha mitaji, ukwasi na yenye kutengeneza faida.

BoT ilieleza kuwa amana na rasilimali za benki ziliendelea kuongezeka Aprili 2023 sambamba na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha kwa njia kidijiti.

“Aidha, ubora wa rasilimali za mabenkiv uliendelea kuimarika, ukiakisiwa na kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu na kufikia asilimia 5.45 mwezi Aprili 2023, ikilinganishwa na asilimia 8.25 mwezi Aprili 2022,” ilieleza.

Taarifa ilieleza kuwa Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia BoT iendelee kutekeleza sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la kiwango cha ukwasi katika uchumi kwa Mei na Juni mwaka huu.

“Utekelezaji huu wa sera ya fedha unalenga kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5.4 katika kipindi kilichosalia cha mwaka 2022/23, na kufanikisha kufikiwa kwa malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF chini ya Mpango wa ECF kwa mwezi Juni 2023,” ilieleza BoT.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live