Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT yabanwa agizo la Samia riba za mikopo

38509d179bcae32c233a0f1fbeba794b BoT yabanwa agizo la Samia riba za mikopo

Thu, 8 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Fedha na Mipango imeiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itekeleze haraka maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba taasisi za fedha zipunguze riba za mikopo.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Yussuf Masauni alitoa agizo hilo jana alipotembelea BoT, Dar es Salaam na kuzungumza na uongozi wa benki hiyo.

Masauni alipongeza jitihada za BoT kukutana na wadau ili kuhakikisha kuwa taasisi za fedha zikiwemo benki na watoa huduma wa sekta ndogo ya fedha wanapunguza riba za mikopo.

“Ikiwezekana mwishoni mwa mwezi huu wananchi waanze kuona matokeo ya juhudi hizo kwa riba kuanza kupungua kwa kuwa kupungua kwa riba ni jambo linalowezekana”alisema.

Aliitaka BoT iweke mikakati kuongeza akiba ya fedha za kigeni kwa kuwa na mbinu za kibunifu zikiwemo za kununua na kuhifadhi dhahabu, kuongeza uuzaji wa bidhaa za Tanzania nje ya nchi na kusimamia shughuli za utalii.

Kuhusu fedha za wananchi waliokuwa wateja wa Benki ya FBME Limited aliitaka BoT ihakikishe wateja wa benki hiyo wanarejeshewa fedha haraka baada ya kukamilisha taratibu za kisheria zinazoendelea Cyprus.

FBME iliwekwa chini ya uangalizi wa Bima ya Amana za Wateja inayosimamiwa na BoT ikiwa katika hatua za kufilisiwa.

Naibu Gavana wa BoT, Dk Bernard Kibesse alisema benki hiyo inakamilisha mazungumzo na benki ili washushe riba kama alivyoelekeza Rais Samia jijini Mwanza.

Alisema wanaendelea kurekebisha kanuni za mikopo zinazotolewa na BoT kwa benki ili kuziongezea ukwasi zitumie fursa hiyo kushusha riba za mikopo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz