Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BoT waeleza jinsi ya kuhifadhi fedha zisiharibike

46716 Bot+pic

Thu, 14 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ngara. Watanzania wameshauriwa kutunza na kuhifadhi fedha za noti na sarafu katika mazingira safi na salama ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuzunguka katika taasisi mbalimbali.

Ushauri huo umetolewa leo Alhamisi Machi 14, 2019 na meneja msaidizi wa mahusiano ya umma wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Victoria Msina wakati akitoa semina ya usalama wa fedha katika matumizi ya kila siku kwa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

Msina amesema wananchi wajiepushe na kutunza fedha hizo kwenye vifaa vyenye kutu kama vyuma au vyungu palipo na ubaridi ama unyevunyevu kwani huweza kugandamana na kuharibika ndani ya muda mfupi baada ya kutengenezwa licha ya kutumia gharama kubwa kutengenezwa.

Pia amesema wananchi wachukue tahadhari ya kuepuka kupewa fedha mkononi kutoka kwa wateja badala yake watumiwe kwenye akaunti katika taasisi za kifedha kujihadhari na kupewa noti bandia hasa noti za thamani tofauti.

"Njia rahisi ya kupokea fedha kihalali ni kutumia  akaunti za benki za aina yoyote zinazotambulika au kwenye miamala kupitia mitandao inayotoa huduma za mawasiliano ya simu kuepuka kuibiwa na kutapeliwa hatimaye kupata hasara," amesema Msina.

Naye meneja msaidizi katika kurugenzi za huduma za kibenki, Abdul Dollah amesema usalama wa fedha unatokana na utengenezaji wa aina mbalimbali za madini kama nickel hivyo zinapotunzwa vibaya huharibika kisha kusababisha mchakato mkubwa na gharama kuziondoa kwenye huduma.

Amesema kutengeneza fedha na kuzisafirisha kutoka sehemu moja hadi nyingine ni kati ya Sh500 milioni mpaka Sh1 bilioni na kwamba utengenezaji wa fedha hapa nchini umeanza mwaka 1996, mwanzoni zilitengenezewa mataifa ya nje kutokana na uwezo mdogo wa mitambo ya kazi hiyo.

Amesema katika kutambua fedha halali, zipo baadhi ya alama zinazoonekana kwa kupapasa katika kingo za noti yakiwemo maandishi yenye kutaja BoT, Alama maalum yenye rangi ya dhahabu ambayo hubadilika kuwa kijani inapowekwa kwenye mashine maalum ya uchunguzi.

"Ukimulika noti halali kwa mwanga tarakimu za thamani yake hutokea, ukiwemo mkanda wa thamani na uzi mwembamba wenye maandishi ya BoT na mwaka wa kutengenezwa ikiwemo sura ya hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere," amesema Dolla.



Chanzo: mwananchi.co.tz