Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biteko atoa angalizo kwa makandarasi Rea

Biteko Ataka Miundombinu Ya Umeme Kuboreshwa Kwa Wakati Biteko atoa angalizo kwa makandarasi Rea

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amewakata makandarasi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kuhakikisha wanatekeleza miradi ya umeme kwa wakati kwa sababu wananchi wana kasi kubwa ya kupata maendeleo.

Biteko ametoa kauli hiyo jana Februari 22, 2024 alipowasha umeme katika kitongoji cha Mkangwe, Kata ya Idunda wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Amesema makandarasi ni lazima waongeze kasi ya usambazaji huduma ya umeme kwa wananchi ili wapate maendeleo.

"Tumefikisha umeme hapa lakini kila eneo wanahitaji kwa sababu kasi ya maendeleo ya wananchi ni kubwa, hivyo makandarasi lazima waongeze kasi ya kusambaza huduma hii," amesema Biteko.

“Nimewaambia watu wa Rea, mkandarasi yeyote atakayezembea kupeleka umeme basi atafute shughuli nyingine ya kufanya, hii ya umeme aachane nayo kwa sababu anawachelewesha wananchi kupata maendeleo."

Biteko amesema mkandarasi anayetekeleza mradi katika kata ya Idunda kama kuna mingine maeneo mengine ikamilishe haraka ili wananchi wapate huduma.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema hadi Desemba 2023 vijiji 360 vimepata huduma ya umeme.

Amesema kati ya vitongoji 1,859 mkoani Iringa, vilivyopatiwa huduma mpaka sasa ni 1,234.

Dendego amesema vitongoji 625 vilivyosalia umeme utafika kabla ya mwaka 2025 kwa sababu wameshatenga Sh46.5 bilioni kwa ajili ya vitongoji 301.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kupeleka umeme kwenye migodi mitano mkoani humo na kwamba, Sh2.59 bilioni zitatumika kupeleka nishati hiyo kwenye maeneo hayo.

Awali, Mhandisi Godfrey Chibulunje aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Rea amesema katika Mkoa wa Iringa umeme utapelekwa kwenye miradi minne ya vituo vya afya, pampu za maji, migodini na maeneo ya kilimo.

Katika Jimbo la Mufindi Kusini, amesema vijiji 71 vimepata umeme.

Amesema Sh65 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

Mbunge wa Mufindi Kusini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa Barabara ya Mtwango inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Mkazi wa Mkangwe, Mariam Nyaule ameishukuru Serikali kupitia Rea na Tanesco kwa kuweza kupatikana kwa umeme kwa sababu awali walikuwa wanafuata huduma ya kusaga nafaka katika maeneo mengine.

"Tumewashiwa umeme katika kijiji chetu hata mashine za kusaga nafaka zipo ambazo tulikuwa tunaenda kusaga Kinengembasi, Ikungi na Isimime," amesema.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mkangwe, Dk Ecria Digalo ameipongeza Tanesco kwa kushirikiana na Rea kwa kusogeza huduma ya umeme kwenye zahanati hiyo.

"Tulikuwa hatuna umeme ila sasa tutafanya kazi zetu kwa ufanisi mkubwa,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live