Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biteko ataka maelewano kukuza uwekezaji madini

61dd4c54f9cd0db284fb99e3d24dc799 Biteko ataka maelewano kukuza uwekezaji madini

Sun, 24 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko amezitaka jamii zinazozunguka maeneo ya migodi kutangaza mazuri yanayofanywa na wawekezaji katika sekta ya madini ili kuwatia moyo wa kufanya shughuli za madini.

Dk Biteko alibainisha hayo juzi akiwa katika ziara yake Kijiji cha Kagerankanda Wilaya ya Kasulu alipotembelea mgodi wa Kampuni ya Life Business unaochimba madini ya chokaa mkoani Kigoma.

Alisema migogoro baina ya wawekezaji katika sekta ya madini na wananchi katika maeneo mengi ya migodi imewafanya wawekezaji kupata hofu ya kuwekeza katika uchimbaji wa madini katika baadhi ya maeneo na hivyo kupunguza uzalishaji.

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri na wawekezaji ili kutatua changamoto zinazojitokeza kati yao ili wawekezaji waweze kutekeleza huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi.

Aidha, Dk Biteko aliahidi kuwa changamoto zilizopo za ukosefu wa barabara na ujenzi wa madarasa zitafanyiwa kazi haraka baada ya kutoa maelekezo kwa mwekezaji huyo.

Kwa upande wake, mmiliki wa mgodi huo, Lister Balegele ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), alisema Kampuni hiyo imekuwa ikilipa mapato ya serikali na michango mbalimbali kutokana na mauzo ya madini ya chokaa.

Kuhusu huduma za kijamii, Balegele alisema mgodi unajenga madarasa mawili mpaka sasa katika shule ya sekondari kijijini hapo, umetoa madawati 50 kwa ajili ya shule pamoja na kugawa kompyuta mpya kwa shule ya sekondari na msingi.

Baada ya ziara ya Dk Biteko katika mgodi huo, mwekezaji wa mgodi huo aliahidi kukamilisha barabara na ujenzi wa madarasa hivi karibuni.

Naye Mjiolojia Mwandamizi kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), John Kalimenze alisema serikali kupitia taasisi hiyo itaendelea kufanya tafiti za madini ili iweze kugundua maeneo zaidi kwa ajili ya uchimbaji na kuongeza tija kwa wachimbaji na kuongeza mapato ya serikali.

Mgodi huo kwa sasa unachimba madini ya chokaa na kusafirisha yakiwa ghafi na kuuza katika kiwanda cha Burundi Cement Company (BUCECO) kupitia mpaka wa Manyovu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live