NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka watendaji na watumishi nchini kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Serikali kwani fedha hizo ndizo zinazotegemewa na watanzania katika kuwaletea maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa Septemba 24, 2023 akiwa wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita ikiwa ni ziara yake ya kwanza kufanyika toka ateuliwe na kuapishwa na Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Amesema kuwa, chini ya uongozi wa Rais Samia, kila kitu kilichopangwa kufanyika kinaendelea kufanyika kutokana na fedha anazotoa katika miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115), ujenzi wa Daraja wa Busisi, ununuzi wa ndege, madarasa, vituo vya afya, utalii na miradhi mingine kadha wa kadha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa Mkoa wa Geita wamemshukuru Mkuu wa nchi kwa kumuamini Dk. Doto Biteko katika nafasi hiyo kubwa na adhimu na kwamba wana imani kuwa ataitendea haki nafasi hiyo kutokana na historia yake ya uchapakazi na uadilifu.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesifu juhudi zilizofanywa na Dk. Biteko wakati akihudumu kama Waziri wa Madini na kueleza kuwa amesaidia kuinua mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa nchi na ameahidi kuwa ataendeleza misingi hiyo mizuri ikiwemo ya kufanya utafiti wa madini katika eneo lote la nchi ili wachimbaji wachimbe madini kwa uhakika na hivyo kuongeza mapato ya nchi. -