Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biteko: Sheria mpya ya madini imeleta matokeo chanya

54723 BITEKO+PIC

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya kutungwa kwa sheria mpya ya madini, kulikuwa na minong’ono kuwa huenda ikafukuza wawekezaji kwenye sekta hiyo.

Baadhi ya watu walihisi kuondolewa kwa baadhi ya vipengele vilivyokuwa vikiwabeba wawekezaji na kunyonya maslahi ya taifa kingekuwa kigezo cha kuwakatisha tamaa na kuwaondoa nchini.

Hivi karibuni gazeti hili lilifanya mahojiano maalumu na Waziri wa Madini, Dotto Biteko ambaye pamoja na mambo mengine ameeleza namna sekta hiyo inavyokuwa baada ya uwapo wa sheria mpya.

Katika makala hii tunakuletea mahojiano hayo yaliyofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.

Swali: Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, ni leseni ngapi kubwa za madini zimesainiwa?

Biteko: Kwanza niseme kabla ya wizara hii kuwa inayojitegemea kulikuwa na maombi mengi ya leseni yaliyosimama kutolewa zikiwamo za wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.

Hali hiyo ilitokana na hatua ya Serikali kurekebisha sheria ya madini Julai, 2017 ambapo sheria hiyo ilianzisha tume ya madini ambayo ina jukumu la kutoa leseni za wachimbaji wadogo na wa kati.

Sheria hiyo pia imezitenga leseni za wachimbaji wakubwa ambazo hazitatolewi na tume, bali zitatolewa na Baraza la Mawaziri.

Maombi ya leseni yaliyokuwa yamesimama kwa kipindi hicho ni zaidi ya 12,000 na baada ya uchambuzi tayari Tume ya Madini imeshatoa zaidi ya leseni 7,000 tangu ilipoanza kazi hadi Machi mwaka huu.

Leseni hizo wamepewa wachimbaji wadogo na wa kati na ni matumaini yetu maombi mengine yanayokuja yatafanyiwa uchambuzi na kutolewa.

Swali: Kwa hiyo hakuna mabadiliko yoyote ya ziada kwa waombaji?

Biteko: Kilichobadilika ni kuwa tofauti na zamani ambapo ilikuwa ukiomba ukiwa wa kwanza umeshapata leseni ya uchimbaji madini.

Sasa anapewa mtu mwenye uhakika wa kwenda kuchimba, lengo ni kuwaondoa watu waliokuwa wanachukua leseni na maeneo makubwa lakini hawachimbi, wanachukua kwa ajili ya kutafuta watu wa kuwauzia.

Tunataka pia kuondoa utaratibu wa mtu mmoja kushikilia maeneo mengi. Kwenye kanzi data yetu tulikuta mtu ameshikilia zaidi ya leseni 714 na kati ya zote hizo hakuna hata moja aliyoanza kuchimba.

Swali: Serikali ilitunga sheria mpya ya madini na rasilimali za Taifa mwaka 2017, kuna changamoto au mabadiliko gani katika kuzisimamia?

Biteko: Hakuna changamoto za kiutekelezaji zaidi ya mtazamo kwa sababu ni kitu kipya na kuna watu hawapendi kitokee hususani ujio wa sheria mpya wakihisi utapunguza wawekezaji.

Waliokuwa wanahisi hivyo wamekosea sana kwa sababu imeleta matokeo chanya zaidi, ambapo kwa miaka 29 hapa nchini hatujawahi kusaini mikataba mikubwa ya madini ‘Special Mining Licence’ (SML) ambayo uwekezaji wake ni wa dola 100 milioni za Marekani.

Hizi leseni kwa sasa maombi yake yapo tumeshayafanyia kazi yapo matatu, kutoka kwa wawekezaji wa nje, wamekuja

kwenye kipindi hiki hiki cha uwapo wa sheria mpya ambayo wengi walikuwa na hofu nayo.

Aina za uwekezaji huo wa SML ni kama ule wa Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara ambao kwa hapa nchini haujafanyika kwa muda mrefu.

Sisi kama wizara tumejiridhisha wamekidhi vigezo vyote na ikimpendeza Mungu hizo leseni zitatoka, siwezi kuzungumzia sana ni lini kwa sababu lipo kwenye ngazi za juu.

Walioomba walikuwa kama 27, tulipowaambia waje kwa ajili ya mawasilisho ya uwekezaji wao walikuja 15 na baada ya mchujo wakabaki hao watatu.

Swali: Katika sheria hiyo mpya, Serikali na nchi inanufaikaje?

Biteko: Manufaa ni mengi, lakini kikubwa ni kuwa nchi itanufaika kwa sababu kila mahali penye uwekezaji Serikali inapata asilimia 16, kodi ya ukaguzi asilimia moja na mrabaha kutoka asilimia tano hadi sita ili kuongeza manufaa.

Haya yote yatainufaisha nchi na kumnufaisha mchimbaji mdogo na mwekezaji.

Bado tunafanya mabadiliko ya sheria mara kwa mara ikigundulika kuna ugumu wa utekelezaji ili kuhakikisha wawekezaji wanapata manufaa na nchi pia.

Kulikuwa kunatengenezwa woga usiokuwa na maana, kwa sababu baada ya kuwapo kwa sheria hiyo ndiyo mapato yameongezeka na wawekezaji pia.

Kuna maeneo kama Kabanga Nikol, Ngwena, Panda Hill wanataka kuchimba madini ya Niyobia ambayo hayajawahi kuchimbwa kabisa, lake Tanganyika kote huko watu wanataka kuwekeza tena uwekezaji mkubwa, achilia mbali wanaotaka kuwekeza kwenye madini ya vito, kuonyesha kuwa wengi wameielewa hiyo sheria na wanataka kuwekeza.

Swali: Kwenye uwekezaji kuna changamoto yoyote?

Biteko: Changamoto iliyopo ni wawekezaji wengi kuja kuwekeza kwa mgongo wa Watanzania wenzetu ambao hawawapi utaratibu mzuri.

Kinachofanyika wanaingia mikataba kinyemela na baadaye wale wageni inaonekana waliibiwa, jambo ambalo ni la aibu na fedheha kubwa.

Hata hivyo, wawekezaji wameanza kuelewa na baadhi ya nchi zimekuwa zikiandaa utaratibu wa kuja na watu wao.

Mfano ubalozi wa Canada, Urusi, India, China, wakiangalia fursa za watu wao kuwekeza hapa nchini kwenye sekta ya madini.

Nia yao siyo kuwaminya wawekezaji bali ni kukamilisha lengo la ‘win win situation’ (haki sawa) Watanzania wapate na mwekezaji apate, tuondoe rushwa na urasimu ili kufanya kazi ipasavyo.

Swali: Kutokana na mikataba mibovu iliyokuwapo awali, Tanzania haikunufaika sana na madini yake. Hilo limebadilika kwa kiasi gani sasa?

Biteko: Baada ya marekebisho ya sheria mapato yameongezeka kutoka kwenye migodi mikubwa na midogo na Watanzania wamelindwa.

Wawekezaji walikuwa wanaamua kutoa fedha ya kusaidia shughuli za kijamii kwenye eneo la uwekezaji (CSR) ambayo lazima ithibitishwe na halmashauri gharama ya kitu unachotaka kukifanya ambapo zamani ilikuwa mwekezaji anajenga darasa kwa Sh17 milioni kesho hata akisema ametumia Sh100 milioni hakuna aliyekuwa anaweza kuhoji.

Walikuwa wanaamua wenyewe wakitaka wanafanya, wasipotaka wanaacha, lakini sheria mpya imeliwekea msisitizo hilo na jinsi ya ufuatiliaji.

Kutokana na hilo miji mingi yenye uwekezaji imebadilika kumekuwa na maendeleo kwa mfano mji wa Geita, Bukombe, Chato kote huko mkono wa mgodi unaonekana.

Tunataka hali hiyo iendelee kwenye migodi mingine yote, mikataba tuliyokuwa tunaingia zamani ilikuwa inawapa uhuru mkubwa wawekezaji, baada ya sheria mpya hali imebadilika sana.

Swali: Unadhani kuna haja ya kupitia upya mikataba ya awali?

Biteko: Nasisitiza kusema kuwa bado tunahitaji kuangalia utaratibu wa kupitia upya mikataba.

Ndiyo maana ilitungwa sheria ya kujadiliana mikataba yenye masharti hasi ili tuweze kuipitia na tuangalie cha kufanya, ni imani yangu Serikali itaendelea kuyapitia yale yote ambayo yataonekana kuwa na upungufu kwenye mikataba hiyo.

Lengo ni kuhakikisha mwekezaji hapati usumbufu lakini na wao watuachie tija kama nchi.

Swali: Kwa miaka mitatu iliyopita, sekta ya madini imechangia kiasi gani kwenye uchumi wa Taifa?

Biteko: Kwa mwaka zilikuwa zikikusanywa Sh196 bilioni pekee kwa madini yote, sasa kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 tulikusanya maduhuli ya Sh310 bilioni.

Kumekuwa na ongezeko kubwa na kwa mwaka wa fedha 2019/2020 tumewekewa malengo ya kukusanya Sh475 bilioni.

Hatukuwahi kufanya hivyo kwa miaka yote, nakuambia tunaweza kukusanya zaidi ya hapo kwa sababu uwezo ni mkubwa.

Kinachotakiwa kufanyika ni kudhibiti wizi, utoroshaji, uaminifu wa wachimbaji wetu, mikataba isiyokuwa na ‘dili’ ndani yake, mapato yataongezeka.

Ukuta Mirerani waja na neema

Swali: Baada ya ujenzi wa ukuta Mirerani na kuzinduliwa kwa soko la madini mkoani Geita, nini kinafuata?

Biteko: Uwekezaji wa kujenga ukuta Mirerani umekuwa mwarobani kwenye sekta ndogo ya madini ya tanzanite.

Baada ya Serikali kujenga ukuta udhibiti umeimarika, na nilitarajia baada ya Tanzanite One kuacha uzalishaji na ukuta kujengwa mapato yangeanguka, lakini ni tofauti kabisa mwaka 2017/18 wachimbaji wadogo wamechangia Sh1.4 bilioni na mwaka huu wa fedha uliopo wameshafikisha Sh1.1 bilioni.

Hapo nyuma kwa wachimbaji wote wakubwa na wadogo mwaka 2016 walikusanya tanzanite yenye uzito wa kilo 147 mwaka uliofuata kilo 166 baada ya ukuta kujengwa wanakusanya kilo 784, hiyo haijawahi kutokea.

Swali: Kwenye huu ukuta kuna changamoto yoyote?

Biteko: Changamoto kubwa ni baadhi ya Watanzania wachache kutokuwa waaminifu, wanaiba madini. Tunawakamata sana hata Aprili 24, tumemkamata mtu akitaka kutorosha.

Udhibiti umeongezeka manufaa yamekuwa makubwa sana pengine tofauti hata nilivyotarajia, lakini wachimbaji wa Mirerani wamekuwa wepesi sana kuelewa, chama cha wachimbaji wadogo na wachimbaji nawaomba waendelee kutoa ushirikiano.

Tunachofanya sasa ni kuhakikisha tunawaondolea kero mbalimbali ikiwamo za kuombwa rushwa.

Ndiyo maana tunasisitiza ujenzi wa masoko kama alivyoagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufikia Juni 30 mwaka huu kila mkoa uwe na soko la madini.

Tumepata soko la Geita na madini yanayouzwa pale ni mengi sana.

Kwa sasa pale wanapata ushuru wa huduma ule wa asilimia 0.5 wanakusanya Sh15 milioni kwa siku ambalo hapo awali lilikuwa pato la mwaka mzima.

Masoko yakiwepo tutazuia utoroshaji na tutawasaidia wenye madini kuepukana na matapeli wanaonunua dhahabu yao kwa bei ndogo.

Swali: Sheria ya mwaka 2017 iliagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhifadhi madini kama akiba ya Serikali. Utekelezaji wake upoje?

Biteko: Tulivyoanza kusimamia sheria hii Rais John Magufuli alielekeza benki kuu waanze kununua dhahabu, lakini kwa sheria yake dhahabu wanayotakiwa kununua lazima iwe na ubora wa kuanzia asilimia 95. Dhahabu nyingi ya wachimbaji wadogo ubora wake ni asilimia 60, 80 na 90, ni kidogo sana.

Rais akaelekeza turuhusu watu waanze kujenga mitambo ya kuyaongezea thamani madini, tukaita watu waombe zabuni walikuja wengi sana wakafanya mawasilisho wakachagua na maeneo.

Baada ya uchambuzi kwa kukubaliana nao kwa kigezo hiki unakidhi, hiki hukidhi wakabaki watano ambao wapo katika hatua ya kuomba leseni.

Miongoni mwao walikuja wakitaka leseni kisha wakatafute fedha ya kujenga, wanataka kuchukua wakafanye biashara ya leseni hatutaki watu wa namna hiyo tunataka anayekuja kuwekeza kabisa.

Waombaji walikuwa mchanganyiko katika hao waliopata wa ndani ni wawili na waliobaki ni wa nje.

Wachimbaji wadogo kuchangia zaidi

Swali: Mchango wa madini kwenye pato la taifa bado ni chini ya asilimia tano na mpango wa Serikali ni kufikisha asilimia 10 mwaka 2025. Kuna mkakati gani unaandaliwa kufikia malengo hayo?

Biteko: Kweli sekta imepangiwa ikifika mwaka 2025 ifikie asilimia 10, hivyo ili kufikia huko lazima utambue vyanzo vya kukufikisha huko.

Chanzo kikubwa ni wachimbaji wadogo ambao waliachwa nyuma, walikuwa hawasaidiwi wanajiendesha wenyewe.

Tulichofanya ni kuanza kuwapatia maeneo ya kufanyia kazi, mengi yalikuwa yanashikiliwa na wawekezaji kutoka nje ambao walikuwa wanasubiri wachimbaji wadogo wapate madini kisha ndiyo wanakuja.

Rais amesema hapana, wachimbaji wadogo wamilikishwe maeneo na kuwapatia masoko wakimaliza kuchimba wajue wanauza wapi.

Jambo lingine ni kuwasaidia masuala ya utafiti ambao katika uchimbaji wa madini ndiko kwenye gharama, sasa tumewafanyia utafiti na taarifa tukawapa, tumejenga vituo maalumu vya kuwafundisha uchimbaji wa kisasa kwenye mikoa kama saba.

Tumejenga migodi ya mifano huko Kantente, Rwamgasa nia ni kuwasaidia waweze kukua na kuongeza uchumi wao, wakiongeza mapato na uchumi wao, utaonekana moja kwa moja kwenye uchumi mkubwa wa nchi.



Chanzo: mwananchi.co.tz