Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bilioni 2.2 zilivyorejesha MV Kitunda, kurahisisha usafiri Lindi

Mtz15 1 Bilioni 2.2 zilivyorejesha MV Kitunda, kurahisisha usafiri Lindi

Tue, 12 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SEKTA ya uchukuzi inatoa mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo ya uchumi, pia ni mwezeshaji mkubwa wa sekta za uzalishaji, biashara na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la kitaifa na kimataifa.

Usafirishaji wa bidhaa na huduma katika masoko, hutegemea zaidi mfumo wa uchukuzi wenye tija na ufanisi kwa ajili ya uhimizaji na uwezeshaji wa biashara na hivyo, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuokoa muda.

Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi, ambapo katika miaka ya hivi karibuni umekuwa na kasi kubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Lindi una jumla ya wakazi 864,652, huku nusu ya wakazi hao wakiishi katika maeneo ya pembezoni kuzunguka Bahari ya Hindi na wananchi hao kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za kijamii kutokana na maeneo hayo kukosa usafiri wa uhakika.

Miongoni mwa maeneo yaliyokuwa yakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri ni Kijiji cha Kitunda kilichopo Manispaa ya Lindi ambao awali wananchi wake walikuwa wakitumia vyombo visivyo salama vya usafiri ikiwemo mitumbwi, ngalawa na majahazi kwa ajili ya kuingia na kutoka eneo la Manispaa ya Lindi kutafuta huduma za kijamii.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ilitekeleza ahadi iliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli aliyoitoa kwa wananchi wa Manispaa ya Lindi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, ilijenga kivuko cha M.V Kitunda kinachotoa huduma ya usafiri wa abiria, magari na mizigo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na MAELEZO, Meneja wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Locky Sabigoro, anasema kivuko hicho kilianza kazi rasmi mwezi Machi 2018, ambapo Serikali ilifanya maboresho ya miundombinu mbalimbali yenye thamani ya Tsh Bilioni 2.2.

Aidha, Sabigoro anasema kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh bilioni 1.9 zimetumika kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara ya kuingilia katika eneo la Kivuko na Sh milioni 333 zimetumika kwa ajili ya kujenga maegesho na barabara na kuongeza kuwa Serikali imetumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya uhakika ya kivuko.

Mhandisi Sabigoro anasema kivuko cha M.V Kitunda kina uwezo wa kubeba abiria 100 na mizigo yenye uzito wa tani 50 pamoja na magari sita kwa wakati mmoja na inatumia muda wa dakika 10 hadi 12 tofauti na wakati wa nyuma ambapo walikuwa wanatumia zaidi ya saa moja kwa ajili ya kuvuka kuelekea upande wa pili.

“Kivuko hiki cha M.V Kitunda kina uwezo wa kubeba abiria 1,800 kwa siku lakini kwa idadi ya wakazi waliopo katika eneo la Kitunda-Manispaa ya Lindi unakuta kivuko kinabeba abiria 500 hadi 600 kwa siku, tumezungumza na Serikali ya mkoa kuona namna bora ya kujenga vivutio vya uwekezaji,’’ anasema Mhandisi Sabigoro.

Akifafanua zaidi Sabigoro anasema Serikali ya mkoa tayari imeanza maandalizi ya kujenga miundombinu ya huduma za kijamii ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa shule na vyuo vya elimu ya juu katika eneo la Kitunda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Kijiji cha Kitunda na kurahakisha kasi ya ukuaji wa maendeleo ya Mkoa wa Lindi.

Mhandisi Sabigoro anasema hapo awali hali ya mawasiliano ya usafiri baina ya wananchi wa Kitunda na Manispaa ya Lindi haikuwa nzuri kwani wakazi wa maeneo hayo walilazimika kutumia mitumbwi na maboti kwa ajili ya kuvuka upande wa pili kwa ajili ya kupata huduma muhimu za kijamii, ambazo nyingi zinapatikana eneo la Manispaa ya Lindi.

Anaongeza kuwa kwa sasa wananchi wanafurahia huduma ya kivuko cha MV Kitunda kutokana na kutumia muda mfupi kuvuka katika eneo hilo hivyo, TEMESA Mkoa wa Lindi imejipanga kuhakikisha inalinda miundombinu ya kivuko hicho ili kuleta maendeleo endelevu kwa ustawi wa wananchi wa Manispaa ya Lindi.

“Rais aliona namna watu walivyokuwa wakihangaika hususani kina mama, walikuwa wakidhalilika na wakati ule magari yalikuwa yanazunguka upande wa pili wa eneo la mnazimmoja na kusafiri umbali wa kilometa 70 kuingia eneo la Kitunda, lakini kwa sasa hali ni tofauti usafiri umekuwa rahisi na kutoa unafuu mkubwa kwa wananchi,’’ anasema Mhandisi Sabigoro.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live