Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bilioni 1.6/- kugharimia mafunzo ya sukari

C851b89b72d137592edd74c7df0941a2 Bilioni 1.6/- kugharimia mafunzo ya sukari

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MFUKO wa Maendeleo wa Tasnia ya Sukari (SIDTF) umeidhinisha Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya kugharimia huduma za mafunzo na uendeshaji wa shughuli za Chuo cha Taifa cha Sukari, kuhakikisha nchi inajitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Akizungumza juzi na wadau wa tasnia ya sukari, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, alisema nchi itarajie mabadaliko makubwa, kwani chuo hicho (NSI) cha pekee katika Afrika Mashariki na Kati kinachoandaa wataalamu wa teknolojia ya sukari, kinatarajiwa kurejea katika kutoa mafunzo Septemba mwaka huu.

Miongoni mwa wadau waliohudhuria mkutano huo jijini Dodoma ni Bodi ya Sukari, Wizara ya Kilimo, wakulima wakubwa na wadogo wa miwa na wazalishaji sukari.

Kusaya alisema ukosefu wa wakufunzi, uchakavu wa vitendea kazi vya kuendesha mafunzo na kuchakaa kwa miundombinu ya chuo, kulisababisha kusimama kwa utoaji wa mafunzo ya kilimo cha miwa na uzalishaji sukari kwa muda mrefu.

Alisema juhudi za serikali na wadau wa tasnia ya sukari za kukiimarisha zimeshaanza na kwamba zinaendelea kufanyika kiwe bora na kinachotoa mafunzo ya kilimo cha miwa na uzalishaji sukari nchini.

Katibu Mkuu alisema juhudi za Serikali na wadau zimewezesha chuo hicho kupata kibali cha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kutoa mafunzo kwa ngazi ya Astashahada na Shahada ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.

Mkuu wa Chuo hicho cha Taifa cha Sukari, Aloyce Kazimili alisema wapo walimu lakini hawakusomea taaluma ya kilimo cha miwa. Aliomba serikali iwasomeshe katika eneo hilo, iwe rahisi kuajiriwa mara kibali cha ajira kitakapotolewa.

Kusaya alimuagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kilimo, kuwapa uhamisho wa muda watumishi wawili wa Kitengo cha Ugavi na Manunuzi na Mkaguzi wa Ndani, irahisishe hatua za awali za kuhuisha uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Sukari .

Aliwaahidi wadau walioshiriki mkutano kuwa atahakikisha ukarabati unaanza mara moja kwa kutumia wataalamu wa ndani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz