Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 8/- kuboresha biashara migebuka, dagaa

8c36fa43bd93d89dd7f7cb22d2198b89.png Bil 8/- kuboresha biashara migebuka, dagaa

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA ni miongoni mwa nchi 10 kati ya 79 za Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacifi c (OACPS), zilizochaguliwa kunufaika na mradi wa zaidi ya Sh bilioni nane (Euro milioni tatu) kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani wa samaki.

Mradi huo kupitia Mfuko Maalumu wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EDF11 for Intra-ACP Projects), utatekelezwa mkoani Kigoma kwa kipindi cha miaka mitano na unahusu samaki aina ya migebuka na dagaa kutoka Ziwa Tanganyika.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilieleza kuwa Tanzania imechaguliwa kunufaika na mradi huo wa thamani zaidi ya Sh bilioni nane.

“Mradi huo utatekelezwa mkoani Kigoma kwa kipindi cha miaka mitano na kusimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) ambapo wavuvi wadogo watapatiwa ujuzi wa kuongeza uzalishaji.

“Watasaidiwa kupunguza upotevu wa mazao ya samaki, kuwezesha mazao ya samaki kufika kirahisi katika masoko ya ndani na n je na utunzaji wa mazingira kuwezesha uvuvi en- delevu na wenye tija,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 kati ya 79 za OACPS zilizochaguliwa kutekeleza mradi huo, unaojulikana kama Fish- 4ACP utakaotekelezwa kwa gharama ya Euro milioni 40 kupitia mfuko wa EDF11 wa miradi ya Intra-ACP.

Mbali na Tanzania, nchi nyingine kwa upande wa Afrika ni Cameroon, Ivory Coast, Nigeria, Sao Tome, Senegal na Zimbabwe. Kwa upande wa Caribbean na Pacific ni Jamhuri ya Dominica, Guyana na Visiwa vya Marshall.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kupatikana kwa mradi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli wakati akizindua Bunge la 12 alipoagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi za Tanzania nje ya nchi, kuhakikisha sekta ya uvuvi inatoa mchango katika kukuza pato la Taifa, ajira na kupambana na umasikini.

“Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji imeomba kibali kutoka Umoja wa Ulaya kuruhusu dagaa wa Kigoma kuuzwa katika Soko la Ulaya ambapo tayari kampuni moja ya Kitanzania imekwishaingia makubaliano ya kuuza tani 20 za dagaa kila mwezi nchini humo,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa upatikanaji wa kibali ukikamilika, dagaa wa Kigoma watauzwa kwa wingi katika nchi mbalimbali za Ulaya kama ilivyo kwa minofu ya sangara.

Chanzo: habarileo.co.tz