Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 680/- zatumika kuboresha Reli ya Kati

A3a13f6b54ad71d8dee3424ca3627bcd Bil 680/- zatumika kuboresha Reli ya Kati

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI kupitia Shirika la Reli Nchini (TRC) inatekeleza mradi wa uboreshaji wa Reli ya Kati kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Isaka mkoani Shinyanga, umbali wa Kilometa 970, kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 680.

Hatua hiyo imelenga kuhakikisha unakuwepo usafiri wa uhakika na kuaminika na kuongeza mwendokasi wa treni kutoka wastani wa sasa wa kilometa 35 mpaka 70 kwa saa.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Msimamizi wa Timu ya Ukarabati kwa kipande ya Isaka hadi Itigi, Bernard Mbonde kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora wakati wakikagua utekelezaji wa mradi huo.

Alisema mradi huo una mikataba 71 ikiwemo minne ya ukarabati wa njia ya reli kuanzia Dar es Salaam hadi Isaka, ununuzi wa mabehewa 44, ununuzi wa vichwa vitatu vikubwa, ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kisasa ya mawasiliano ya kuongozea treni na ununuzi wa mtambo wa marekebisho ya njia ya reli.

Mbonde alisema vichwa vitatu na mabehewa 44, yatawasili nchini wakati wowote mwezi huu na yataongeza ufanisi katika usafishaji wa mizigo na abiria.

Alisema sehemu ya pili ya mradi, ambayo kwa kiasi kikubwa iko mkoani Tabora, njia za reli zilizobadilishwa kwa kuondoa reli ndogo na kuweka reli nzito ni kilometa 45.5. Sehemu hiyo ni kutoka Igalula hadi Tabora. Njia za reli zilizokarabatiwa ni kilometa 125 na sehemu hiyo ni kutoka Itigi hadi Tabora

Mbonde aliongeza kuwa njia za kumpuzikia treni, zimerefushwa katika stesheni mbalimbali kutoka mita 400 hadi 600 ili kuwezesha treni ndefu kupumzika kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Hassan Wakasuvi aliitaka TRC kurudisha utaratibu wa zamani wa uendeshaji na usimamizi wa shirika hilo, ikiwemo kufufua magenge ambayo yatasaidia kuimarisha ulinzi na kuhakikisha usafishaji wa miundombinu.

Alisema kukosekana kwa watumishi reli katika magenge mengi, miundombinu ya reli iko hatarini kuhujumiwa na kuharibiwa na mifugo na wakulima wanaolima kando ya reli, kwa kuwa hakuna mtu anayesimamia kipande kati ya stesheni moja na nyingine.

Mwenyekiti huyo alilitaka shirika hilo kuongeza idadi ya watumishi ili kuwepo na usafiri katika maeneo mbalimbali ya stesheni, ambapo katika baadhi ya vituo kama vile Itulu kuna mfanyakazi mmoja.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati aliwataka wawekezaji kwenda mkoani humo, kuwekeza katika shughuli mbalimbali, kwa kuwa sasa hivi njia ya reli iko vizuri. Alisema TRC inatarajia kuongeza mabehewa ambayo yatawezesha wawekezaji kusafirisha bidhaa zao kwa gharama za chini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz