Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 3/-kusambaza mkonge mikoa 17

CvmaiuuXYAEJN59 Bil 3/-kusambaza mkonge mikoa 17

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imetoa Sh bilioni 3/- katika mwaka wa fedha 2020/21, kuongeza utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za mkonge zitakazogawiwa kwa wakulima kwenye mikoa 17 inayolima zao hilo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ametoa kauli hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga kufuatilia maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoyatoa Juni mwaka huu kwa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano kulifufua zao la mkonge.

"Serikali ya Awamu ya Tano tayari imekipatia Kituo cha Utafiti TARI Mlingano shilingi bilioni 3 za kukiwezesha kuongeza utafiti na uzalishaji mbegu bora zenye kutoa mavuno mengi ambazo zitagawiwa kwa wakulima wa mkonge nchini,"alisema Kusaya.

Kusaya alisema lengo la Wizara ya Kilimo ni kuona Kituo cha TARI Mlingano kinazalisha mbegu bora milioni tano mwaka huu 2020/21 ili zigawiwe kwa wakulima waongeze uzalishaji wa mkonge kutoka tani 36,000 za sasa kufikia lengo la tani 120,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Mkurugenzi wa TARI Mlingano, Dk Catherine Senkoro alimhakikishia Kusaya kuwa wameanza kutekeleza agizo hilo kwa kuongeza eneo linalolimwa mbegu kutoka hekta mbili za sasa hadi hekta 65 .

"Jumla ya hekta 65 zimelimwa ambapo kati yake hekta 15 zimepandwa miche ya mkonge ipatayo 1,500,000 kufikia mwezi Agosti mwaka huu," alisema.

Dk Senkoro aliiomba Wizara ya Kilimo kuendelea kukiwezesha kituo hicho kuwa na maabara ya kisasa, ili kiongeza kasi ya utafiti wa mbegu bora za mkonge kwa njia iitwayo "Tissue Culture Laboratory" inayotoa matokeo mazuri na mbegu nyingi.

Alisema mahitaji ya mbegu bora za mkonge kwa wakulima wadogo nchini kwenye mikoa yote 17 inayolima yamefikia 1,200,000, wakati lengo la wizara ni kuzalisha mbegu bora 5,000,000 kwa mwaka.

Dk.Senkoro alitaja pia mafanikio ya Kituo cha TARI Mlingano kuwa ni kuwafundisha kanuni bora za kilimo cha mkonge maofisa ugani 427. Pia kimetoa mafunzo kwa wakulima 22,000 wakati wa Maonesho ya Kilimo Nanenane mkoani Simiyu ikishirikiana na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).

Kusaya aliitaka menejimenti ya TSB kufanya Sensa ya Wakulima wa Mkonge na kiasi cha eneo wanalolima ili mashamba yasiyolimwa wizara ishauri serikali kuyatwaa na kuwapa wawekezaji wenye uwezo.

Kusaya aliielekeza Bodi ya Mkonge Tanzania kusimamia malipo ya wakulima wa majani ya mkonge, wanaodai kutolipwa na AMCOS na pia kudhibiti vitendo vya baadhi ya wakulima kuvuna mkonge usiokomaa na kuharibu ubora unatotakiwa.

Katika ziara hiyo, Kusaya aliipongeza TSB kwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kuhamia kwenye jengo la Mkonge House jijini Tanga.

"Nimefurahi leo kuona Bodi imehamia kwenye jengo hili la Mkonge House kama alivyoagiza Waziri Mkuu, sasa nataka mfanye kazi kubwa kusimamia uongezaji uzalishaji wa mkonge kwa wakulima zaidi kuhamasishwa kulima ili ardhi yote iliyokusudiwa kupandwa mkonge ilimwe," alisema Kusaya.

Katika hatua nyingine, Kusaya alisema tayari serikali imetoa fedha Sh milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ofisi ya bodi hiyo ili liwe bora, baada ya kutwaliwa kutoka kwa mwananchi aliyemilikishwa kinyume na utaratibu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Saad Kambona alisema tayari kazi ya usajili wa wakulima wa mkonge imeanza. Alisema kuwa wakulima 7,551 wadogo wa mkonge, wamesajiliwa kwenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Morogoro.

Kambona alisema TSB itaendelea kuhamasisha na kuelimisha wakulima wengi, kuanzisha mashamba mapya ya mkonge na kupanda mbegu bora ili uzalishaji uweze kukua zaidi.

Kusaya pia alitembelea Kiwanda cha Kuzalisha Mbolea cha ABM Tanga, kukagua uzalishaji wa mbolea.

Chanzo: habarileo.co.tz