Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil. 3/- kusambaza mbegu za michikichi

Fwedha Bil. 3/- kusambaza mbegu za michikichi

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Assa Makanika.

Katika swali lake, mbunge huyo alihoji serikali haioni umuhimu wa kuwekeza yenyewe katika zao la michikichi badala ya kuziachia halmashauri ili kukabiliana na upungufu wa mafuta nchini.

Bashe akijibu swali hilo, alisema katika kipindi cha mwaka 2019/20 hadi mwaka 2020/21, imewekeza Sh. bilioni 5.8 kwa ajili ya kuendeleza zao la michikichi.

Aidha, alisema hadi kufikia Januari 31, mwaka huu, jumla ya miche bora ya michikichi 2,244,935 imezalishwa na jumla ya miche 1,456,111 imesambazwa kwa wakulima katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kigoma.

“Miche 788,824 inatarajiwa kusambazwa kwa wakulima katika msimu wa 2020/2021,” alisema.

Naibu Waziri huyo alisema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa tani 570,000 kwa mwaka.

Hata hivyo, alisema uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufikiwa wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka, ambapo hupelekea nchi kutumia wastani wa kiasi cha Sh. bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka.

“Kama ilivyo kwa mazao mengine, serikali huwekeza katika utafiti, uzalishaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, huduma za ugani, udhibiti wa visumbufu vya mazao na utafutaji wa masoko,” alisema.

Aidha, alisema katika utekelezaji mikakati hiyo, serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo Mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi.

“Kama sehemu ya mkakati wa kujitosheleza kwa mafuta ya kula, mwaka 2018 serikali iliamua kuanzisha kituo maalum cha utafiti wa zao la michikichi cha TARI Kihinga mkoani Kigoma ili kuendeleza zao hili kwa ufanisi zaidi,” alisema.

Alisema TARI Kihinga inashirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), halmashauri na sekta binafsi katika utafiti, uzalishaji wa miche bora ya michikichi na kuisambaza kwa wakulima.

“Serikali itaendelea kushirikisha wadau wa sekta ya umma na binafsi kuendeleza zao la mchikichi na mazao mengine ya mbegu za ili kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula,” alisema.

Chanzo: ippmedia.com