Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 3.7/- kujenga masoko ya samaki

E838d910e01456c21ac3e5f14710d5ec Bil 3.7/- kujenga masoko ya samaki

Mon, 5 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI itatumia zaidi ya Sh bilioni 3.7 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa mialo na masoko kwa kuweka miundombinu ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kupunguza upotevu.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, alisema hayo jana Dar es Salaam katika Mkutano wa Uongozi wa Soko la Samaki la Ferry, wavuvi na wafanyabiashara wa eneo hilo kuzungumzia maboresho ya soko hilo yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Ndaki alisema ingawa idadi ya wavuvi inakadiriwa kufikia milioni 4.5 nchini, serikali imekuwa haipati pato la kutosha kutoka sekta hiyo.

Alisema wizara yake imejipanga kuweka mazingira rafiki ya kibiashara katika masoko yote na mialo ya kupokelea samaki ili kuongeza tija katika sekta ya uvuvi nchini.

"Lengo ni kuhakikisha tunawawezesha wavuvi kuongeza ufanisi na tija katika kazi yao sambamba na kuongeza mchango wao katika pato la taifa ambalo mwaka huu ni asilimia 1.7, tunakusudia siku zijazo hili likue zaidi," alisema Ndaki.

Alisema asilimia 95 ya wavuvi nchini ni wadogo wanaovua samaki kwa ajili ya matumizi ya chakula na asilimia tano iliyobaki wanavua kwa ajili ya biashara, hivyo serikali imeweka mkakati ili kuwainua.

"Rais Samia Suluhu aliilekeza wizara kuboresha mazingira na miundombinu ya uvuvi ili kuwawezesha wavuvi na wafanyabiashara kuchangia pato la taifa," alisema Ndaki.

Alisema asilimia 30 hadi 40 za mazao ya samaki yanapotea kutokana na kutokuwapo kwa miundombinu ya uhifadhi na kwamba, kufanyika kwa ukarabati huo kutawezesha samaki hao kuhifadhiwa kwa viwango bora.

“Lengo ni kuhakikisha mazingira ya soko hili lililojengwa kwa msaada wa Japan yanakuwa na viwango bora likihusisha mitambo ya kutengeneza barafu na mengineyo,” alisema.

Aliutaka uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha unaushikirisha uongozi wa wafanyabiashara na wavuvi katika mchakato mzima wa ujenzi ili kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija aliwataka wavuvi na wafanyabiashara kuushirikiana na mkandarasi ili akamilishe kazi hiyo kwa wakati.

Alisema ujenzi huo utakaofanyika kwa awamu utawalazimu wafanyabiashara hao kusogea kutoka maeneo ya ujenzi na kutengewa maeneo mengine hadi utakapokamilika ndiyo warejee.

Chanzo: www.habarileo.co.tz