Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 27/- za EU kutumbukizwa kwenye ufugaji nyuki

F4c96d362f2a39a9f35245ee3d4cc0e1 Bil 27/- za EU kutumbukizwa kwenye ufugaji nyuki

Tue, 22 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imezindua programu ya kuwezesha mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki ambao utatekelezwa kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) uliotoa Euro milioni 10 sawa na Sh bilioni 27.

Programu hii ambayo inafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) itatekelezwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Shinyanga na Pemba.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mary Masanja ambaye alisema kwa sasa serikali inafanya uchambuzi wa kitaalamu kubaini wilaya na vijiji vilivyomo ndani ya mikoa hiyo ambapo mradi huu utatekelezwa.

Alisema programu hiyo inakwenda kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa mazao ya nyuki, kuwezesha maeneo ya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya nyuki, kujenga uwezo wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na taasisi zinazosimamia sekta hii.

Pia kuwezesha taasisi za utafiti wa nyuki kwa kuweka vitendea kazi katika maabara ya utafiti iliyopo Njiro mkoani Arusha na kuweka mfumo thabiti itakayowezesha ufanyaji wa biashara ya mazao ya nyuki.

Masanja alitumia fursa hiyo kuwasihi wakuu wa mikoa ambayo programu hii inatekelezwa kutoa ushirikiano unaostahili na kusaidia kufafanua jambo hilo kwa wananchi.

Pia Masanja amemuelekeza Katibu Mkuu, Dk Francis Michael kushirikiana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe kutenga maeneo yatakayotangazwa kuwa hifadhi za nyuki ili wananchi na wawekezaji waweze kutumia kwa ajili ya ufugaji nyuki kibiashara.

Pia ameagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuwaelekeza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya hususani kwenye mikoa yenye fursa kubwa ya ufugaji nyuki kuajiri maofisa ufugaji nyuki watakaotumika kutoa huduma kwa wananchi.

Masanja pia ameelekeza maofisa wa nyuki wote wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoa mafunzo na huduma za ugani kwa wafugaji nyuki walio katika maeneo mbalimbali hapa nchini na wizara ishirikishe wadau waone namna bora ya kukusanya takwimu katika sekta ya ufugaji nyuki.

Kwa upande wa Balozi wa Ubelgiji hapa Tanzania, Peter Van ACKER alisema Umoja wa Ulaya umetoa ufadhili huo ili kuisaidia Tanzania kutumia fursa ya soko la asali la Umoja huo.

"Nchi za Ulaya zinazalisha asali inayotosheleza kwa asilimia 60 ya mahitaji, hivyo ni fursa kwa Tanzania kuchangamkia soko la Ulaya kwenye soko la asilimia 40 hasa ikizingatia Tanzania inashika nafasi ya pili Afrika katika uzalishaji mazao ya nyuki nyuma ya Ethiopia."

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania, Manfredo FANTI alisema Tanzania ina fursa ya kutumia soko la Ulaya kufanya biashara kwenye mazao ya kilimo na mifugo ikiwamo mazao ya nyuki bila ushuru au tozo kutokana na mikataba ambayo Tanzania imeingia na Umoja huo.

Awali Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Francis Michael alitoa hakikisho kuwa Wizara iko tayari kuratibu usimamizi na utekelezaji wa programu kwa maslahi mapana ya Taifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live