Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 11/- zapungua simu za nje ya nchi

B51449387c8794c85f805c3fda06f4dd.jpeg Bil 11/- zapungua simu za nje ya nchi

Thu, 18 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema mapato kutokana na simu za nje ya nchi yamepungua kutoka zaidi ya Sh bilioni 25 kwa mwaka hadi Sh bilioni 14.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile alisema kutokana na hilo, serikali kupitia TCRA inataka kufanya tathmini kufahamu chanzo cha kupungua kwa mapato na hali hiyo inachangiwa kiasi gani na upigaji wa simu kupitia mitandao ya kijamii.

Dk Ndugulile kwa nyakati tofauti alisema jijini Arusha kuwa, serikali haijatangaza kuwa itaweka tozo ili kudhibiti upigaji simu nje ya nchi kwa kutumia mitandao hiyo.

Aliyasema hayo jijini humo alipotembelea ofisi za taasisi zilizo chini ya wizara hiyo likiwemo Shirika la Simu Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania, na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Pia juzi asubuhi wakati anazungumza kwenye kipindi cha Morning Trumpet cha kituo cha televisheni cha U TV kinachomilikiwa na kampuni ya Azam Media alizungumzia jambo hilo.

“Hatujatoa kauli kwamba tunakwenda kuzizuia wala hatujasema kwamba tutaenda kweka tozo katika jambo hili kwa hiyo lengo ni kutaka kupata takwimu ambazo zinaweza kutusaidia na sisi kupata uelewa zaidi katika jambo hili,” alisema Dk Ndugulile wakati akizungumza kwenye kipindi cha Morning Express cha kituo cha redio cha U FM cha Dar es Salaam.

Mitandao kadhaa ya kijamii inatumika nchini ukiwemo wa Whatsapp, Facebook, Instagram, Youtube, Twitter, na Telegram.

MAELEKEZO KWA KAMPUNI ZA SIMU

Dk Ndugulile alisema, Machi 2, mwaka huu serikali ilitoa maelekezo kwa kampuni za simu kwamba kuanzia Aprili 2 mwaka huu zianze kutumia bei elekezi za vifurushi.

“Kwa mara ya kwanza mwananchi anaweza akamgawia mwenzake ‘data’ pale anapoona kwamba hawezi akaitumia, lakini tumeweza kutoa maelekezo kuhusiana na ukomo wa wa vifurushi,” alisema.

Alisema kampuni za simu pia zimepewa maelekezo kuhusu matangazo yanayotumwa kupitia simu za wateja na pia ziwe na app ili mteja afuatilie matumizi ya intaneti katika simu yake.

“Marekebisho haya yanahitaji mabadiliko makubwa sana katika mifumo ya mtoa huduma ndio maana tumetoa ifikapo Tarehe Mbili Mwezi wa Nne, ni lazima kampuni zote ziwe zimetekeleza hili,” alisema Dk Ndugulile na kuziagiza kampuni za simu zisitumie kipindi cha mpito kuwanyonya wateja wao kwenye huduma za intaneti.

Aliiagiza TCRA ipitie upya tozo kwa wanaotoa maudhui mitandaoni wakiwemo wenye redio na televisheni ili ziwe rafiki.

“Tanzania tuna tatizo la content, maudhui, sasa hebu tupunguze kidogo. Hawa vijana wametafuta kamera yake, wametafuta nini vyombo vyake sasa tunapomuwekea gharama kubwa sana tunamkosesha fursa hawa vijana wetu hivyo mkafanye na mapitio hizo tozo zenu. Naamini ni mamlaka ya waziri mtaniletea nitaziangalia…” alisema Dk Ndugulile.

AONYA MAFUNDI SIMU

Alionya mafundi simu wanaofuta namba za IMEI (International Mobile Equipment Identity) za simu za mkononi za wateja wao ili simu hizo zitumike tena.

Dk Ndugulile alisema kitendo hicho ni kosa kisheria na kwamba serikali itaitumia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010 kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya hivyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz