Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bidhaa tatu zawa pasua kichwa

Bidhaapiic Data Bidhaa tatu zawa pasua kichwa

Tue, 5 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya bidhaa mbalimbali nchini kupanda bei kutokana na sababu tofauti, bidhaa tatu muhimu za chakula zimeonekana ni pasua kichwa na kusababisha kilio kikubwa cha wananchi, Mwananchi limebaini

Bidhaa hizo ni pamoja na mbili zilizotajwa hivi karibuni na Tume ya Ushindani (FCC) wakati ikitoa onyo kwa wazalishaji, waagizaji na wasambazaji nchini – sukari na mafuta ya kula.

Ukiacha sukari na mafuta ya kula, ngano ni bidhaa nyingine ambayo haina utulivu wa bei hivi sasa, hali inayowatisha waokaji na walaji wa bidhaa zitokanazo na zao hilo.

FCC ilitoa onyo hilo baada ya kupokea malalamiko ya bidhaa hizo kuuzwa kwa bei kubwa kiasi cha baadhi ya wananchi kushindwa kuzimudu.

Malalamiko hayo yanatokea katika kipindi ambacho vita kati ya Russia na Ukraine inaendelea, hali inayoiyumbisha dunia kiuchumi na kibiashara.

Kutokana na umuhimu na mahitaji ya bidhaa hizo, Safina Suleiman mkazi wa Kunduchi anasema kupanda bei kwa mafuta na ngano kunahitaji kutazamwa kwa jicho la kipekee kwa kuwa hivi karibuni imekuwa ikiongezeka karibia kila siku.

Advertisement “(Awali) Ilikuwa kama huna hela ya kutosha kununua mchele, unanunua ngano upike chapati kwa mlo (labda) wa usiku, lakini sasa hivi unga wa ngano na mafuta ni ghali kuliko mchele,” alisema Safina.

Safina anaungwa mkono na mamalishe wa jijini Dar es Salaam, Beldina Amoni aliyesema bei ya unga wa ngano imepanda mpaka Sh2,000 kutoka Sh1,500 kwa kilo, hivyo amelazimika kuongeza bei ya vitafunwa anavyotengeneza.

“Chapati niliyokuwa nauza Sh300 sasa ni Sh400 ili nisipate hasara, maana bidhaa nyingi yakiwamo mafuta na sukari zimepanda bei,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Waokaji Tanzania, Ally Rwendura alisema maumivu ya kupanda bei ya ngano, mafuta ya kula na sukari wameanza kuyahisi huku bei ya mikate ikiendelea kubaki ileile, japo viwango vinabadilika.

“Maumivu yalianza tangu wakati wa mlipuko wa Uviko-19, kiroba cha kilo 25 za ngano tuliyokuwa tunanunua Sh28,500 mwaka 2020 kiliongezeka hadi Sh38,000 ila tumeambiwa mwezi ujao itaongezeka kwa Sh3,000 zaidi kutokana na vita vinavyoendelea,” alisema Rwendura.

Kwa kuwa biashara lazima iendelee, Rwendura alisema hofu yake ni uwezekano wabidhaa zao kupungua ubora ili kuendana na hali halisi.

“Mkate unatakiwa kuwa na uzito wa gramu 500 (nusu kilo) lakini hivi sasa kuna wanaotengeneza hadi wa gramu 280 ili mradi kumudu gharama za uendeshaji, unakuta mkate umejaa hamira tu, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mlaji,” alisema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Bakhresa Group, Hussein Sufian alinukuliwa hivi karibuni akisema vita vya Russia na Ukraine vimeongeza bei ya ngano na kufika dola 500 kwa tani kutoka chini ya dola 480 iliyokuwapo kabla ya mlipuko wa Uviko-19.

Badala ya kupata ngano Russia ambako ilikuwa nafuu, Sufian alisema sasa hivi Tanzania inanunua ngano kutoka Marekani, Canada, Argentina, Ujerumani na Australia ambako gharama ziko juu.

Mipango ipo

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema jitihada zinafanyika kuongeza uzalishaji wa ngano nchini.

“Mwaka jana tulianza kwa kugawa mbegu kwa wakulima wa kanda ya kaskazini ambako tulipeleka zaidi ya tani 200, mwakani tutagawa tena ili kufufua zao hilo,” alisema Bashe.

Bashe alisema huko nyuma nchi ilikuwa inajitosheleza kwa kati ya asilimia 70 hadi 80 lakini kilimo hicho kilikufa kutokana na kukosekana mfumo thabiti wa kuwalinda wakulima.

“Sasa tuna makubaliano na wakulima, mwaka jana walinunua mbegu kwa kati ya Sh900 hadi Sh1,000 kwa kilo na sasa tumeanza kilimo cha mkataba katika baadhi ya maeneo,” alisema Bashe.

Waziri huyo alifafanu kwamba kuanzia mwaka ujao, Wakala wa Mbegu (ASA) utaanza kuzisambaza na kukiwa na upungufu zitaagizwa nje ili kukidhi mahitaji.

Hapa nchini, ngano inalimwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara na Serikali inakusudia kuyatumia mabonde ya Bahi na Mbarali kwa ajili ya kilimo hicho na majaribio yameanza ili wakulima wakivuna mpunga, wapande ngano inayokomaa ndani ya siku 78.

Sukari nayo...

Kama ilivyo ngano, sukari nayo vilevile inapanda, lakini kilio chake hapa nchi ni cha muda mrefu.

Fimbo Butallah, mkuu wa Idara ya Biashara wa kampuni ya Kilombero Sugar, anasema bei ya sukari duniani inazidi kupanda kutokana na kukosekana kwa kontena na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine.

Anasema kampuni yake imepewa kibali cha kuagiza sukari nje kufidia upungufu unaokuwepo kila mwaka, lakini ana wasiwasi huenda bei ikawa juu sokoni tofauti na ambavyo wamekuwa wakinunua siku za nyuma.

Alisema wanaangalia pia Uganda, sukari ikipatikana huko huenda kukawa na unafuu wa bei kwa kuwa hakuna changamoto za usafiri na athari za vita hazijafika huko.

Akizungumzia sukari, Bashe alisema miongoni mwa bidhaa za chakula ambazo nchi inatumia fedha nyingi kuagiza kutoka nje ni sukari, na ndio maana Serikali inasaidia viwanda vya ndani kumaliza changamoto zilizokuwepo ili kupanua uwekezaji wao.

“Serikali kwa kushirikiana na kiwanda cha Kilombero kuna uwekezaji mkubwa umefanyika wa zaidi ya Sh540 bilioni, hatua hii itawafanya kuongeza uwezo wao kutoka tani 110,000 za sasa hadi tani 270,000, hivyo sukari itaongezeka kwa wastani wa tani 140,000,” alisema.

Bashe alisema hivi sasa kuna mradi wa tani 10,000 ambao unatarajia kuanza katika Wilaya ya Mtwara Vijijini wenye thamani ya Sh11 bilioni lakini pia Serikali imeisaidia kampuni ya Lift Valley kuwekeza Sh10 bilioni katika kiwanda kitakachozalisha tani 10,000.

“Tunatarajia kufikia Julai mwaka huu kiwanda cha Bagamoyo Sugar kianze uzalishaji wa tani 35,000 za sukari lakini pia Mkulazi II ipo kwenye hatua za mwisho kuzalisha tani zaidi 50,000 na kuna kiwanda kingine Morogoro cha kuzalisha tani 4,000, hivyo matarajio ni kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani,” alisema.

Waziri Bashe alisema Serikali kupitia Bodi ya Sukari Tanzania na taasisi nyingine za utafiti wanakusudia kuwa na viwanda vidogo vya sukari na mambo yakienda vizuri Juni mwaka huu kiwanda cha kwanza kitaanza uzalishaji na kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 10 za miwa.

“Ukienda Kilombero wakulima wanazalisha miwa, mingine inabaki haitumiki. Kuwa na viwanda vidogo vidogo katika maeneo ya kuzalisha miwa maana yake wakulima watakuwa na uwezo wa kuwekeza katika viwanda hivyo kwa kulima, kuchakata na kuuza,” alisema Bashe na kuongeza kuwa lengo ni ili kufikia 2025 Tanzania iwe miongoni mwa wauzaji wa sukari nje.

Mafuta ya kula

Hii ni moja ya bidhaa zizotumika mno nchini, mahitaji ya mafuta ya kula kwa mwaka ni zaidi ya tani 570,000 wakati uzalishaji wa ndani ukikadiriwa kuwa tani 210,000.

Kwa mahitaji hayo, nchi inatumia zaidi ya Sh470 bilioni kuagiza tani 360,000 kutoka nje ya nchi kila mwaka.

Hali hiyo inanfanya Athuman Mbuti, mkaanga kuku eneo la Tabata Relini, Dar es Salaam asema katika miezi ya karibuni, bei ya mafuta ya kula imepanda mara dufu kutoka Sh3,000 kwa lita moja hadi Sh6,500 kwa lita hivyo kupunguza faida.

Hata hivyo, anasema “bado nauza kuku bei ileile, hizo gharama nazibeba. Uzuri ni kwamba mafuta unatumia zaidi ya mara moja lakini gharama zikiendelea huenda ikaondoka na faida yote, hapo itabidi tupandishe bei ili mtaji usikate. Sasa hivi ukimwona mtoto anachezea mafuta unaweza kumzaba kibao,” alisema Mbuti.

Akizungumzia mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, Bashe aligusia eneo hilo akisema Tanzania ina nakisi ya mafuta na hivyo imeamua kuanza na mradi wa majaribio wa kugawa mbegu bora za alizeti ili kuongeza uzalishaji wa ndani.

“Mwaka huu tumesambaza tani 1,600 kwa wakulima shambani na wameuziwa kwa bei ya ruzuku ya Sh3,000 kwa kilo, tofauti na bei iliyozoeleka ya Sh7,000 hadi 35,000 kwa kutegemea na aina ya mbegu, msimu ujao wa kilimo tutagawa tani 5,000,” alisema Bashe.

Aprili 2021 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliliambia Bunge kuwa ili kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula Serikali inatekeleza mikakati ya kufufua zao la chikichi ambalo limeonekana kuwa na ufanisi mkubwa katika uzalishaji wa mafuta ya kula.

Mbali na mchikichi Majaliwa alisema mikakati hiyo inakwenda sambamba na kuimarisha uzalishaji kwenye mazao mengine ya mbegu ikiwemo alizeti, nazi na pamba ili kupata mafuta mengi na kujitosheleza.

Bei haiepukiki

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe alisema kuongezeka kwa bei ya bidhaa mbalimbali kutokana na vita vinavyoendelea kati ni jambo ambalo haliepukiki kama Rais Samia alivyolieleza, lakini Serikali inafanya juhudi za kupunguza athari.

Alisema kwa bidhaa zinazotokana na mazao ya kilimo Wizara ya Viwanda na Biashara inafanya kazi kwa karibu na ile ya Kilimo kuhakikisha kilimo kinakuwa cha tija ili kuviwezesha viwanda vya kuongeza thamani kuwa na uzalishaji wa kutosha.

“Katika bidhaa kama ngano, miwa na alizeti tunapigia chapuo kilimo cha mkataba ili kuongeza tija katika uzalishaji kwa ajili ya viwanda vyetu, baada ya hapo tunashughulika na usambazaji kuhakikisha hakuna kuongeza bei kiholela,” alisema Kigahe.

Alisema “wakati kunapoibuka changamanoto kama hivi, kuna wafanyabiashara wanaongeza bei bila sababu za msingi kwa kuwa wamepata kisingizio na hilo tunalidhibiti kupitia FCC.”

Alisema suluhisho la kudumu la kuleta utulivu wa bei katika bidhaa hizo tatu hata zinapotokea changamoto mbalimbali ni kuvutia uwekezaji mkubwa, mdogo na wa kati katika kilimo na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo huku Serikali ikiweka mazingira ya kuvutia na kulinda uwekezaji huo.

Aibu kubwa

Balozi mstaafu Ami Mpungwe ambaye ni mdau katika biashara tofauti zikiwemo za kilimo na viwanda, alisema changamoto zinazoteteresha usambazaji na bei ya mazao ni kengele ya kuarifu umuhimu wa kujitosheleza.

“Nikiangalia ngano, sukari na mafuta ya kupikia ni bidhaa ambazo nchi yetu inaweza kujitosheleza, tuna ardhi nzuri ya kutufanya kuzalisha mazao hayo pengine kuliko hata nchi za Russia na Ukraine, kuendelea kutegemea bidhaa hizo kutoka nje ni aibu,” alisema Balozi Mpungwe.

Alisema nchi yenye uwezo wa kuzalisha zao fulani la chakula haitakiwi kuchezea fursa hiyo kwa kuwa mahitaji ya chakula yapo na yanaongezeka kila siku kwa kuwa watu wanazidi kuzaliwa.

Akitolea mfano sukari alisema hakuna jambo linaloshindikana kuwa na uzalishaji unaotosheleza mahitaji, kilichokuwa kinakosekana ni mazingira yanayovutia wawekezaji katika eneo hilo.

“Suala la kuvutia uwekezaji si katika sukari tu ni katika bidhaa zote muhimu,” alisema.

Jambo zuri ni kuwa hivi sasa kuna mazingira ya kisiasa, kiuchumi na ya kiuwekezaji yanayotia matumaini, ni muda wa kuvuta watu kuja kuwekeza katika maeneo hayo, wawekezaji wapo na mitaji yao, ni kuwaita tu,” alisema Mpungwe.

Akisisitiza kauli yake ya kengele ya tahadhali, alisema ni rahisi kucheza na mazao ya biashara na athari zisiwe kubwa, lakini si mazao ya chakula au yanayotengeneza chakula, Serikali inapaswa kuvutia uwekezaji kwa wingi na haraka katika eneo hilo.

Mtaalamu wa Uchumi Dk Abel Kinyondo alisema matukio yanayotokea ulimwenguni hayasababishi changamoto ya upatikanaji wa huduma na bidhaa katika nchi yoyote, isipokuwa yanadhihirisha tatizo lililokuwepo.

‘Changamoto za ulimwengu zinaonyesha upungufu uliokuwepo, hata nishati ya mafuta tunayotegemea zaidi inapotokea changamoto inatuonyesha kuwa hatujatumia vyanzo vyetu vya nishati ipasavyo kama mbadala wa nishati hiyo,” alisema.

Dk Kinyondo alisema suluhisho la kudumu katika changamoto za bidhaa mbalimbali tulizonazo au ambazo huwa zinajitokeza ni kuangazia mapungufu na kuyatafutia majibu ya ndani.

“Ukiangalia kuna tatizo, ardhi tuliyonayo na fursa ya uzalishaji lakini kila likitokea jambo lolote bidhaa hizo zinatikiswa kwa bei na usambazaji wake, linalojitokeza ndilo linalokuwa sababu,” alisema.

Alisema suala la kutegemea baadhi ya bidhaa hususani za chakula kutoka nje wakati kuna ardhi ya kutosha kuongeza uzalishaji wa ndani, hayo ni matatizo yetu ya ndani na dawa yake ni kuongeza uwezo kuzalisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live