Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara ya vitalu vya uwindaji yadoda

43806 Pic+utalii Biashara ya vitalu vya uwindaji yadoda

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Vitalu vya uwindaji wa kitalii 71 kati ya 159 vilivyopo nchini vimerudishwa na wawekezaji licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanyamapori kutokana na sababu mbalimbali ikiwapo kuyumba kwa biashara ya uwindaji wa kitalii.

Akizungumza na Mwananchi jana mjini hapa, kamishna mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini (Tawa), Dk James Wakibara alisema kwamba hadi sasa kuna vitalu 82 vipo wazi na wawekezaji wanakaribishwa.

Alisema vitalu 77 ndiyo vina wawekezaji ambao wanafanya uwindaji wa kitalii na upigaji picha na 11 havijapata wawekezaji tangu vilipotangazwa.

Hata hivyo, alifafanua kwamba kubaki wazi kwa vitalu hivyo kumechangiwa na sababu mbalimbali ambazo hazihusiani na mabadiliko ya sheria mpya ya umiliki wa vitalu ambavyo sasa vitakuwa vikiuzwa kwa mnada.

Alisema kwamba licha ya baadhi ya vitalu kuwa wazi, Tawa imeweza kudhibiti matukio ya ujangili na hivyo vitalu hivyo vina idadi kubwa ya wanyama.

“Haya maeneo ya vitalu kuna wanyama wengi lakini ni makubwa hivyo si rahisi kudhibitiwa kirahisi katika kukabiliana na ujangili lakini tumeweza kudhibiti,” alisema.

Kwa upande wake, naibu kamishna wa Tawa ambaye anashughulikia masuala ya uhifadhi na ujangili, Misungwi Mabula alisema kwamba ili kuboresha mifumo ya ulinzi wa mapori ya akiba na mapori tengefu ambayo yapo chini ya mamlaka hiyo wanaandaa mkakati wa ulinzi kufuata ikolojia.

Wakati huohuo, Takukuru inamshikilia mkurugenzi wa kampuni ya wawekezaji kutoka Falme ya Kiarabu ya Ortello Business Cooperation (OBC), Isack Lesion Mollel kwa uchunguzi siku chache baada ya kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwapa kazi raia 10 wa kigeni bila kufuata taratibu.

Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha, Frida Wikes jana alitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa uchunguzi wa tuhuma za Mollel unaendelea hata hivyo hakuzitaja.

“Tumekuwa tukipokea maswali kutoka kwa waandishi juu ya kumshikilia bwana Mollel kwa taarifa hii tunathibitisha kuwa ni kweli kuwa Takukuru mkoa wa Arusha inamshikilia mkurugenzi mtendaji huyo wa kampuni ya Ortello Business Corporation limited(OBC) kwa ajili ya chunguzi unaoendelea dhidi yake,” alisema

Mkurugenzi huyo anashikiliwa siku chache baada ya kufikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka 10 ya kuwapa kazi raia wa kigeni 10 katika kambi za kampuni hiyo Loliondo kinyume cha sheria. Wafanyakazi hao ambao wapo nje kwa dhamana walikuwa wakifanyakazi ya kuandaa mapokezi ya Mfalme wa Dubai ambaye anatarajiwa kutembelea nchini hivi karibuni.



Chanzo: mwananchi.co.tz