Miaka 38 iliyopita Michael Aldrich, mfanyakazi wa kampuni ya Tesco nchini Uingereza aligundua mfumo wa kompyuta wa kuwezesha miamala kati ya wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa.
Ugunduzi wa Aldrich ambao baadaye ulikuja kujulikana kama biashara kwa njia ya mtandao (E-commerce) kwa wakati huo haukuwa na thamani na sehemu kubwa ya watu ulimwenguni walikuwa hawafikirii kama siku moja wangefanya manunuzi kupitia kompyuta au simu wakiwa wamekaa sebuleni kwao.
Tangu kugunduliwa kwa huduma hiyo, biashara ya mtandaoni taratibu ilianza kuzoeleka na kuchukua sehemu kubwa ya muda na matumizi ya watu na kufanikisha kuibuka kwa kampuni kubwa zinazofanya biashara ya mtandaoni ikiwemo Amazon na E-bay.
Benki ya Umoja wa Madola ya Australia inakadiria kuwa hadi kufikia 2013 biashara ya mtandao ilifikia asilimia sita au Dola 257 bilioni ya biashara zote za Marekani ambapo nchini Uingereza pekee ilikuwa inachangia asilimia 39 ya ukuaji wa sekta ya bidhaa za rejareja.
Mwenendo wa kuchangamkia fursa hiyo ya teknolojia haukuwa mkubwa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hivyo kufanya watu wengi kuendelea kununua bidhaa na huduma kwenye maduka ya kawaida maarufu mjini kama “Kwa Mangi”.
Licha ya kuwepo kasi ya kobe hapo awali katika utumiaji wa teknolojia, Tanzania nayo kwa sasa inaibukia katika huduma ya biashara ya mtandaoni baada ya kampuni kama Jumia Tanzania, Kupatana, Zoom Tanzania kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali kwa kompyuta na simu za kisasa zilizounganishwa na intaneti.
Hata hivyo, ikilinganishwa na baadhi ya mataifa ya Kenya, Afrika Kusini au Nigeria muitikio wa biashara ya mtandaoni bado sio mkubwa kwa watanzania licha ya idadi ya watu wanaomiliki simu na kutumia mtandao wa intaneti kuongezeka kwa kasi.
Takwimu mpya za robo ya kwanza ya mwaka 2018 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa watumiaji wa simu za mkononi wamefika 40.3 milioni. Idadi hiyo imefanya watanzania takribani milioni 23 kufikiwa na huduma za intaneti.
Meneja Uhusiano wa Jumia, Godfrey Kijanga anasema biashara kwa njia ya mtandao bado ni ngeni miongoni mwa watanzania wengi kutokana na kuzoea mifumo ya asili ya manunuzi ambayo imejengeka katika jamii kwa muda mrefu.
“Watanzania wengi bado wamekumbatia mifumo yao ya asili ya kufanya biashara na manunuzi. Wafanyabiashara bado wanategemea wateja kuja moja kwa moja madukani mwao na wateja nao bado wanaamini ili kupata bidhaa sahihi lazima uione, uiguse, uikague au kuichunguza pamoja na kuijaribu kama ikibidi,” anasema Kijanga.
Kasi ndogo ya matumizi ya mtandao kufanya biashara au manunuzi ni matokeo ya kutokuwa na uelewa juu ya fursa zilizopo katika teknolojia hiyo.
Mtaalamu wa mifumo ya manunuzi kutoka kampuni ya Innovify Tanzania, Florian Kaboda anabainisha kuwa muamko mdogo wa watu kutumia huduma ya biashara ya mtandaoni unatokana na watanzania wengi kutogundua fursa zilizopo mtandaoni ambazo zinaweza kurahisisha maisha.
“Hata kama watumiaji wa intaneti wameongezeka, watu wengi hawajui fursa zilizopo wanaishia kwenye mitandao ya kijamii tu. Tunapasa kuitokomeza fikra ya aina hiyo,” anabainisha Kaboda.
Matumaini ya biashara ya mtandaoni kujiimarisha na kuwafikia watanzania wengi bado yapo ikizingatiwa kuwa teknolojia inakuwa kwa kasi na hakuna namna zaidi ya watanzania kukubaliana na mifumo mipya ya biashara.
“Hii ni ishara nzuri kwetu sisi na biashara kwa ujumla, tunaamini kuwa wateja wa sasa ni waelewa na wanakwenda na wakati, hivyo suala la kuchagua kutumia teknolojia itakayorahisisha maisha yao haliepukiki,” anabainisha Kijanga.
Kwa mujibu wa Kijanga, idadi ya wateja wanaotembelea mtandao wa Jumia imeongezeka kutoka wateja 250,000 mwaka 2017 hadi kufikia wateja 500,000 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ikiashiria kuwa watanzania wengi wameanza kutambua faida za biashara ya mtandaoni.
Kitu gani kinawavutia watu kutumia biashara ya mtandaoni?
Katika nchi zilizoendelea duniani, inakadiriwa watu 77 kati ya 100 wameunganishwa na huduma ya intaneti.
Mpenyo huo mkubwa wa intaneti ambao unawawezesha watu kukutana mtandaoni umerahisisha maisha na kuwafanya kubadilishana uzoefu, mitindo wa maisha na tabia ya matumizi ya bidhaa mbalimbali.
Pia, teknolojia ya kufanikisha miamala inakua kwa kasi huku programu nyingi zenye ufanisi na usalama wa juu zikigunduliwa.
Mwanzilishi na Mmiliki wa tovuti ya Daily Life Talk, Jane Shusa anasema kupitia biashara hiyo unaweza kufanya manunuzi ukiwa popote na hauhitaji kufunga safari kwenda kufuata bidhaa dukani jambo linalookoa muda, pesa na kumuhakikishia mtu usalama wake.
“Manunuzi ya mtandaoni yanabadilisha desturi zilizokuwepo, vitu vingi unaweza kununua mtandaoni mpaka matunda, mboga mboga naweza kupata kwa kutumia simu yangu nikiwa popote,” anabainisha Jane.
Kupitia mtandao, mnunuzi ana machaguo mengi ya bidhaa anazohitaji kwa kulinganisha bei, ubora ambapo ni tofauti na bidhaa zilizopangwa kwenye maduka makubwa yanayopatikana maeneo mbalimbali nchini.
Kama mteja hajaridhishwa au amepelekewa bidhaa ambayo haikuiagiza au kutokidhi matarajio yake, kampuni nyingi ikiwemo Jumia zina sera inayomtaka mteja kuirejesha ndani ya siku saba. Bidhaa hiyo pindi inaporudishwa inatakiwa isiwe imefunguliwa au kutumika.
Bashara ya mtandaoni katika nchi za Afrika inafanyika zaidi katika maeneo ya mjini ambako watu wanatumia zaidi intaneti. Changamoto iliyobaki ni uchelewaji wa bidhaa mpaka inapomfikia mteja ambapo huchukua siku moja mpaka saba jambo linawafanya watu wengi kuendelea kutumia maduka ya kawaida.
Kwa wanunuzi wa bidhaa mtandaoni kama Jane bado wanafikiri kuwa changamoto iliyobaki kwa huduma hiyo kukidhi mahitaji ya watanzania ni kupunguza muda ambapo bidhaa imeagizwa mpaka inapomfikia mteja
Pamoja na kwamba teknolojia inatoa fursa lukuki za kufanya manunuzi mtandaoni baadhi wanaona kuna faida nyingi mtu akienda kununua bidhaa dukani.
Peter Edwin, mkazi wa Kimara Suka jijini Dar es Salaam anafikiri kuwa kununua bidhaaa dukani ni njia nzuri zaidi kwa sababu mteja anakuwa na mawanda mapana ya kufanya uchaguzi na kuiona bidhaa kama inafaa au la.
“Kununua dukani ni nzuri tofauti ya mtandaoni ambapo unasubiri zaidi ya siku moja na zaidi uletewe bidhaa yako licha ya kuwa wanakuletea mpaka ulipo,” anasema Peter ambaye amekuwa akifanya manunuzi ya bidhaa zake kwenye maduka makubwa yaliyopo Kariakoo.
Biashara ya mtandaoni ni tishio kwa maduka makubwa?
Kumekuwa na mtazamo tofauti juu ya ujio wa manunuzi ya mtandaoni kwamba yanaathiri biashara ya maduka makubwa kama Mlimani City, City Mall, Choppiers Supermarket yaliyopo nchini kutokana na ongezeko la watu wanaotumia huduma za mtandaoni.
Wamiliki na waendeshaji wa maduka hayo wanaamini kuwa biashara ya mtandaoni haijaathiri mauzo katika maduka yao kwasababu huduma hiyo bado haijapata msukumo mkubwa na watanzania wengi bado wanaamini kwa kuiona bidhaa husika.
Wameieleza Nukta kuwa kutembelea maduka makubwa pia ni sehemu ya utalii wa ndani na mapumziko ya mwisho wa juma. Meneja Mwendeshaji wa Duka la ToyKingdom la Mlimani City, Paul Namuhisa anasema; “kwa Tanzania biashara hiyo sio tishio kwa sababu haijaimarika lakini tunajiandaa kukabiliana na ujio huo.”
Namuhisa ameiambia Nukta kuwa ili kuhakikisha uwepo wa soko la uhakika, wanatengeneza mazingira rafiki ya kuwavutia wateja wengi zaidi kutembelea maduka yao ikiwemo kutumia mbinu ya punguzo la bei.
“Sio kwamba maduka yatafungwa lakini miaka kumi ijayo karibu kila kitu kitakuwa kinapatikana mtandaoni. Tumejiandaa kukabiliana na ushindani huo ili kuhakikisha tunaendelea kuwepo kwenye soko kwa muda mrefu ujao,” anasema Namuhisa.
Kuna dhana kuwa watumiaji wa bidhaa Tanzania na kwingineko barani Afrika ni tofauti ukilinganisha na sehemu zingine duniani kwa sababu wamezoea wanapokwenda kufanya manunuzi wanahakikisha bidhaa wanaiona, wanaishika, kuikagua na wengine kuijaribisha kabisa. Hivyo kuwashawishi watu wote kuhamia mtandaoni itachukua muda.
“Ni kweli mwamko wa watu kuhamia kwenye biashara za mtandaoni ni mkubwa lakini sidhani kama hiyo ni sababu ya kuua mfumo unaotumiwa kwa sasa,” anafafanua Kijanga kutoka Jumia.
Hata hivyo, Kaboda kutoka Innovify Tanzania anashauri kuwa watanzania wanapaswa kujiandaa na mabadiliko makubwa ya teknolojia ya manunuzi ya mtandaoni na kutumia fursa hiyo kuboresha maisha.
Licha ya muitikio mdogo wa watanzania juu ya biashara ya mtandaoni, huko Marekani biashara hiyo imeimarika zaidi ambapo mtandao wa habari wa Business Insider unaeleza kuwa kwa mwaka 2017 zaidi ya asilimia 10 ya manunuzi yalifanyika mtandaoni jambo lililosababisha madukwa makubwa 6,400 kufungwa kwasababu ya kukosa wateja.