Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara usiku kucha Dar sasa mbioni kuanza

Wed, 1 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakazi wa Dar es Salaam wataweza kufanya manunuzi na biashara usiku kucha kuanzia Juni, kama mpango unaofanywa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda utakamilika.

Akizungumza jana wakati wa kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, Makonda alisema biashara zitaanza kufanyika usiku kabla ya mwezi huo kuisha.

Mwaka huu mwezi mtukufu wa Ramadhani unatarajiwa kuanza Mei 5 na kumalizika Juni 4, ambapo Makonda alisema masoko ya usiku yataanza kufanya kazi. “Kila kitu kimeshapangwa. Nataka tuanze kabla ya kuisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani,” alisema mkuu huyo wa mkoa ambaye hata hivyo hakufafanua maandalizi hayo.

Makonda aliwahi kuzungumzia mkakati wake wa kuruhusu biashara kufanyika usiku kuanzia Februari.

Januari 8, akizungumza na wanahabari ofisini kwake, alisema kabla ya Februari ofisi yake ingeruhusu wafanyabiashara kufanya shughuli zao saa 24 wakiwemo wamiliki wa baa.

Alisema ofisi yake iko katika mchakato wa kukutana na wafanyabiashara kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo na kuangalia njia zipi za kuzingatia ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wa kutosha.

“Kabla hatujawaruhusu wafanyabiashara hawa kufanya kazi zao saa 24, kuna mengi ya kuyaandaa hasa kuhakikisha wanajiandaa lakini pia tunafunga taa za usalama na kamera ili kuzuia uhalifu,” alisema.

Hata hivyo, jana alisema kwa sasa anahitaji ripoti kutoka Manispaa ya Ilala ili kujua jukumu walilopewa la maandalizi ya mpango huo limefikia katika hatua ipi. Hata hivyo hakulitaja jukumu hilo.

Pia, alisema wanasubiri upande wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wakamilishe kazi waliyopewa. Alisema kuwa baada ya hapo watamuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutembelea jiji na kwamba, anatamani jambo hilo liwe tayari katika mfungo wa mwezi wa Ramadhani ili Waislamu wakimaliza saumu yao wawe wanakwenda kutembea nyakati hizo.

Wanaodhalilishwa kijinsia

Makonda pia aliagiza mtu yeyote akienda hospitali ama katika vituo vya afya akiwa amelawitiwa au kubaka apokewe hata kama hana hati ya polisi ya PF3 ili ushahidi upatikane.

Alisema kuna wakati wazazi wa watoto wanasumbuliwa wanapokwenda hospitali wakitakiwa kwenda kwanza polisi kupatiwa PF3, kabla ya kupatiwa huduma.



Chanzo: mwananchi.co.tz