Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara Tanzania, Uturuki yafikia Dola milioni 237

82d2f5b7e3bdbadd61bd84f60ce7d232 Biashara Tanzania, Uturuki yafikia Dola milioni 237

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Balozi wa Uturuki nchini, Dk Mehemet Gulluoglu amesema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kilifikia zaidi ya Dola za Marekani milioni 237 mwaka jana.

Katika mahojiano maalumu na HabariLEO jana jijini Dar es Salaam, Balozi Dk Gulluoglu alisema Uturuki na Tanzania wana uhusiano mzuri na wamekuwa wakishirikiana kwenye sekta mbalimbali na kufungua fursa kwa wananchi zikiwemo za biashara, uwekezaji na ajira.

“Kiwango cha biashara mfano mwaka jana kilifika Dola za Marekani milioni 237.48 na Tanzania ilifanya biashara na Uturuki ya Dola za Marekani milioni kati ya 40 na 50,” alisema Balozi Dk Gulluoglu.

Alisema muda mfupi ujao wawekezaji kutoka Uturuki wataanza kuwekeza kwenye sekta ya utalii wa maputo na wamepanga kufanya uwekezaji huo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Akitoa mfano, alisema Uturuki imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya utalii na kwa mwaka 2021 sekta hiyo ilipata watalii milioni 40 waliotembelea taifa hilo.

Alisema mwaka 2020 watu 2,000 walipewa visa kwenda Uturuki kwa ajili ya biashara na mwaka jana idadi hiyo iliongezeka maradufu na kwamba Watanzania 6,800 walipewa visa kwenda nchini humo kufanya biashara.

“Utaona ukuaji wa biashara unaongezeka sio tu kuwekeza bali hata mazingira ya biashara baina ya Uturuki na Tanzania ni mazuri, Watanzania wanapenda bidhaa za Kituruki kutokana na ubora wake vivyo hivyo kwa Uturuki tunanunua bidhaa Tanzania kama viungo,” alisema Balozi Dk Gulluoglu.

Kuhusu kuwekeza nchini, Balozi Dk Gulluoglu alisema wawekezaji wa Uturuki waliosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wengi wao wamewekeza katika viwanda vidogo vikiwemo vya samaki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live