Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara Tanzania, India kufikia Sh17.5 trilioni

Pesa Fedhaddd Biashara Tanzania, India kufikia Sh17.5 trilioni

Fri, 20 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

India imesema inaamini kuwa baada ya ziara ya Rais Samia Suluhu nchini mwao, thamani ya biashara kati yake na Tanzania itaongezeka mwaka huu na kufikia zaidi ya Dola za Marekani 7 bilioni (Sh17.5trilioni) kwa mwaka.

Hayo yameelezwa jana na Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan wakati akizungumza na waandishi wa habari katotika ofisi za ubalozi huo jijini Dar es Salaam, akielezea mafanikio ya ziara hiyo.

Amesema baada ya mataifa hayo mawili kubadilisha aina ya uhusiano wake kutoka uhusiano wa kidiplomasia wa kawaida na kuwa ule wa kimkakati, miongoni mwa athari zake ni kukua kwa biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.

"Wakati nafika hapa mwaka 2021, thamani ya biashara kati ya India na Tanzania ililuwa Dola 2.5 bilioni (Sh6.25 trilioni) mwaka uliofuata ikafika Dola 4.5 bilioni (Sh11.25 trilioni), mwaka wa fedha ulioisha ilifikia Dola 6.4 (Sh16 trilioni) na sasa kwa namna mpya ya uhusiano wetu tunatarajia tutafikia Dola 7 bilioni (Sh17.5 trilioni)," amesema Balozi Pradhan.

Amesema kabla ya ziara ya Rais Samia mara ya mwisho mkuu wa nchi ya Tanzania kutembelea India, ilikuwa miaka nane iliyopita (2015) na Mkuu wa India kutembelea Tanzania ilikuwa mwaka 2016 lakini kwa uhisiano wa kimkakati ulioanzishwa mawasiliano yataboreshwa zaidi nchi zitatembeleana.

"Katika uhusiano wa kimkakati kila nchi itakuwa na maeneo yake ya kipaumbele ambayo yatachukuliwa na kwa uzito," amesema na kuongeza kuwa barani Afrika, nchi ambazo tayari zina uhusiano wa aina hiyo na nchi yake tofauti na Tanzania ni Nigeria, Afrika Kusini na Misri.

Aidha mwakilishi huyo wa India nchini amesema mbali na kukuza thamani ya biashara, ziara hiyo inatarajia kuongeza kiwango cha uwekezaji kutoka katika Taifa lake huku akisema kuwa Serikali za nchi zote zitakuwa tayari kuwezesha hilo.

"Sisi kama Serikali hatutaongeza biashara wala biashara isipokuwa tutawezesha wafanyabiashara wetu kufanya hivyo na kuendelea kuhamasisha wengi zaidi kufanya biashara zinazohusisha nchi hizi mbili," amesema Pradhan.

Balozi Pradhan ametolea mfano wa zao avocado ambalo Tanzania inaweza kuongeza kiwango chake cha biashara kwenda India. "Sisi tumeondoa ushuru wa Avacado kutoka Tanzania lakini bado suala la usafirishaji ni changamoto kwani njia iliyopo ni ya anga tu ambayo inaifanya bidhaa hiyo kuwa na bei ghali lakini pia kusafirishwa kwa uchache"

"Parachichi nyingi za Tanzania zinasafirishwa kupitia Mombasa, Kenya kwa sababu ya miundombinu ya bandari ya Dar es Salaam kutokuwa rafiki kwa kukosa uwezo wa kutunza matunda hayo yasiharibike, sasa kuna ukarabati unaendelea, ukikamilika biashara hiyo itakuwa zaidi kwani kwa meli ni rahisi na nafuu kuliko kusafirisha kwa ndege," amesema.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus amesema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika kukuza ushirikiano ni sekta ya ulinzi hasa utoaji wa mafunzo, nishati na madini ambapo nchi hiyo imeonyesha nia ya kutoa wahandisi wa madini.

Vilevile amesema ushirikiano wa kuimarisha ulinzi wa majini, biashara, kujengeana uwezo, elimu na teknolojia, elimu na mitandao na kuwashirikisha vijana katika masuala ya teknolojia.

Zuhura amesema hayo yatafanyika kupitia hati 15 zilitiwa saini ambapo hati 10 ni baina ya taasisi za Serikali na tano ni Sekta Binafsi.

"Hati hizo za makubaliano (taasisi za Serikali) ni kati ya Wizara ya afya na taasisi za afya za nchi hiyo, makubaliano mengine ni kuimarisha masuala ya kidigitali, ushirikiano wa masuala ya kiutamaduni, kongani za viwanda, kituo cha uwekezaji (TIC) kuweka sahihi na taasisi ya India inayoshughulikia uwekezaji, na kushirikana katika ukarabati wa vyombo vya majini," amesema Zuhura.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live