Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara Rwanda, Tanzania yafikia Tsh. bil 635/-

4ebd0d11a11f0e510dc7cee369f5dbad Biashara Rwanda, Tanzania yafikia Tsh. bil 635/-

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Biashara kati ya Tanzania na Rwanda imefikia Dola za Marekani milioni 274.6 (takribani Sh bilioni 635 za Tanzania) huku nchi hizo zikitakiwa kukabiliana na vikwazo vilivyopo ili kuimarisha usafirishaji huru wa bidhaa na mwingiliano wa watu kati ya nchi hizo.

Aidha, Tanzania imeeleza kutokuwa kikwazo katika changamoto mbalimbali zilizopo za kibiashara zinazoendelea kujadiliwa katika ngazi za juu za uongozi.

Balozi Mdogo wa Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda, Happiness Ruangisa, alisema suala la kutumia vitambulisho vya taifa kama hati za kusafiria kwa watu wanaokwenda Tanzania, visa ya pamoja ya utalii na eneo la mtandao mmoja ni mambo yanayoendelea kujadiliwa na viongozi katika ngazi za juu huku yakiendelea vizuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara ya Afrika Mashariki (EABC), John Bosco alisema kabla ya Covid-19, Kituo cha Mpakani cha Rusumo kilikuwa kinasafirisha malori 400 kila siku.

Kwa mujibu wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Rwanda yamefikia Dola milioni 269.6 wakati mauzo ya Rwanda kwenda Tanzania yamefikia Dola milioni 5.

Katika mdahalo huo, nchi wanachama wa EAC zilitakiwa kuharakisha matumizi ya nyaraka muhimu ili kurahisisha mwingiliano kwa wafanyabiashara wa mipakani katika ukanda wa EAC.

Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC ilitiwa saini na wakuu wa nchi tano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Novemba 20, 2009 ili kuhakikisha usafirishaji huru wa bidhaa, watu, huduma, vibarua na mitaji, matumizi ya sarafu moja kwa shughuli za kila siku ndani ya Soko la Pamoja, shirikisho la kisiasa pamoja na umoja wa forodha.

Lengo kuu la Itifaki ya Soko la Pamoja ni kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kukuza uhusiano wa kijamii wa raia wa Afrika Mashariki kupitia kuondoa vizuizi vya biashara ya kikanda na harakati za raia wa Afrika Mashariki.

Kituo cha Mpakani cha Rusumo kinachounganisha Rwanda na Tanzania pia ni lango muhimu kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo pia inatarajia kuwa mwanachama wa EAC.

Mtaalamu wa Sera kutoka Wizara ya Biashara na Viwanda Rwanda, James Tayebwa, alisema Tanzania na Rwanda zilitia saini mkataba wa kukuza biashara ya mipakani na kuwakaribisha wafanyabiashara kushiriki katika kamati ya pamoja ya mpaka ili kujadili na kuunda mpango madhubuti wa utekelezaji wa makubaliano.

Mjumbe wa Bodi ya Tanzania Women Chamber of Commerce Tanzania, Editha Paschal, aliiomba Serikali kuwawezesha wanawake wa mipakani kupata vifaa vya kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna, kupata mikopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, kuhamasisha juu ya viwango vya bidhaa na kuanzisha huduma za malezi ya watoto karibu na mpaka.

Chanzo: www.habarileo.co.tz