Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara Kenya, Tanzania yafikia yapamba moto

5849642bd6210ec945c2c09c5bbfc071 Biashara Kenya, Tanzania yafikia yapamba moto

Tue, 22 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Biashara kati ya Kenya na Tanzania imefikia Dola za Marekani milioni 905.5 katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2021.

Hayo yamebainishwa na Benki Kuu ya Kenya katika kongamano la uwezeshaji biashara lililoandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) na kufanyika katika Mpaka wa Namanga.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa EABC, John Kalisa, alisema uagizaji wa Kenya kutoka Tanzania ulifikia Dola za Marekani milioni 501 huku wakiuza Dola milioni 403.9.

Kalisa aliwapongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa kutatua baadhi ya vikwazo visivyo vya ushuru vilivyosababisha kuimarika kwa uhusiano bora wa kibiashara baina ya nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Meneja wa Kituo cha Mpaka cha Namanga, alisema malori 250 yanapita katika mpaka huo kila siku, ikiwa ni ongezeko mara tatu kutoka Mei mwaka jana.

Wasafirishaji wa mizigo walitoa mwito wa kutenganishwa kwa Fomu za Tamko la Uagizaji bidhaa kutoka kwa Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Forodha na kuanzishwa kwa skana ya kudumu ya mizigo mpakani ili kurahisisha biashara.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Usafirishaji Kenya, Daniel Wainaina, alisema gharama ya uondoaji wa mizigo upande wa Kenya imepanda kwa asilimia 70 kutokana na michakato na idara nyingi.

Alisema lori la tani 20, gharama yake ni takribani Dola 200 (Sh 22,710) na kusababisha kutokuwa na ushindani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki, Gerald Masila, alisema baraza hilo liliongoza maendeleo ya viwango vilivyowianishwa vya EAC vya nafaka na viwango vya uchukuaji sampuli na upimaji ili kukuza biashara ya mipakani.

Wafanyabiashara hao walitaka watumishi wa ziada kutumwa katika Mamlaka ya Chakula cha Kilimo nchini Kenya ili kuwezesha uidhinishaji wa maombi ya awali ya mahindi kutoka Tanzania na upimaji wa pamoja wa sumu ufanyike Arusha ili kupunguza kiwango cha mahindi yanayokataliwa mpakani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wasagaji Nafaka, Paloma Fernanda, alisema kuna haja ya kampeni ya pamoja ya kukabiliana na sumukuvu kutoka shambani ili kupunguza hasara baada ya kuvuna.

Peter Musiba kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), alisema Tanzania inapambana na sumu ya aflatoxin kwa kuweka vituo vya kupimia maeneo ya Dodoma, Shinyanga na Singida ili kurahisisha biashara ya nafaka.

"Soko la Pamoja la EAC liko hai kupitia kuwezesha biashara," alisema Ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eugenia Mwesiumo.

Alisema mashirika ya kuvuka mipaka yana jukumu muhimu katika kurahisisha biashara.

Kukosekana kwa utambuzi wa viwango vya bidhaa, kushindwa kwa mfumo na kusababisha ucheleweshaji wa utoaji wa hati, vizuizi vingi vya barabarani kwa pande zote mbili na kuharibika kwa skana za mizigo na kusababisha msongamano wa magari ya mizigo ni baadhi ya changamoto zilizotajwa na wafanyabiashara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live