Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bertha: Kutoka ufugaji kuku hadi mwenyekiti SAU

10856 Pic+bertha TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miaka ya nyuma, baadhi ya wanawake nchini walikuwa wanaogopa kujiingiza katika masuala ya siasa badala yake waligeuka kuwa wapiga kura.

Hata hivyo, hali hiyo ilianza kubadilika kuanzia mwaka 2005 hadi kufikia mwaka 2015, ambapo wanawake wengi walibadilika na kuonyesha mwamko wa kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Hali hiyo inachagizwa na mikataba mbalimbali ya kimataifa, sheria na katiba za nchi mbalimbali ambazo zinabainisha haki za wanawake za kushiriki katika shughuli za uchaguzi kwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Miongoni mwa mikataba hiyo ni tamko la kimataifa kuhusu haki za binadamu ambalo linaeleza kuwa binadamu wote wana haki sawa za kisiasa bila ya kubaguliwa kwa njia yoyote ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa kijinsia.

Hata, Baraza la Umoja wa Mataifa linasisitiza haki za wanawake za kisiasa katika mkataba wake wa haki za wanawake za kisiasa uliopitishwa mwaka 1952, Umoja wa Afrika (AU), kwenye tamko la SADC la jinsia na maendeleo la mwaka 2008 na mkataba wa nyongeza wa haki za wanawake wa mwaka 1995.

Lakini mambo yamekuwa mazuri zaidi kwani tumeshuhudia wanawake wengi wakijitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa juu katika vyama vyao, baada ya kuthubutu na kujikubali.

Miongoni mwa wanawake hao ni Bertha Mpata (56), ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau).

Bertha (56), anachukua nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Dk Paul Kyara aliyefariki dunia Desemba 18, 2017.

Hata hiyo, tangu afariki dunia Dk Kyara, chama hicho kimekaa miezi sita bila kuwa na mwenyekiti hadi Juni 30, mwaka huu alipochaguliwa Bertha kushika nafasi hiyo akiwa mwanamke wa pili nchini kushika wadhifa kama huo baada ya Anna Mghwira aliyekuwa ACT-Wazalendo (sasa amehamia CCM).

Mwanamama huyo ambaye ni mfugaji wa kuku anasema alivutiwa na Dk Kyara katika utendaji kazi wake kabla ya kufariki duniani.

Bertha ambaye, kwa sasa ni mwenyekiti pekee mwanamke kushika nafasi ya juu kuongoza chama katika vyama vya siasa nchini, anasema alivutiwa na utendaji kazi wa Kyara na ndiyo sababu ya yeye kujiunga SAU.

Anafafanua kuwa bado kuna vikwazo vingi vinavyowakabili wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hasa katika siasa ikiwemo urasimu, rushwa na mfumo dume.

Uchaguzi

SAU ilifanya uchaguzi wake wa viongozi mbalimbali ikiwemo mwenyekiti, Juni 30, mwaka huu.

Mbali na kuchaguliwa Bertha kuwa mwenyekiti wa SAU, chama hicho kilimchagua Issa Zonga kuwa Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), John Mswanyama (makamu mwenyekiti (Bara) na Kisena Fred Kisena kuwa katibu mkuu.

Mwenyekiti huyo anabainisha kuwa siri ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo inatokana na chama chake kutoa kipaumbele katika suala la usawa wa kijinsia.

“Wanawake wanaweza endapo watapewa nafasi,” anasema Bertha ambaye anasema chama chake kina wanachama zaidi ya 700,000 nchi nzima.

Alivyoanza siasa

Mwanamke huyo ameanza kujihusisha na siasa tangu mwaka 2005 ambapo alijiunga na SAU, baada ya kushawishiwa na aliyekuwa mwenyekiti kwa wakati huo, Dk Kyala miaka 13 iliyopita.

Anabainisha kuwa anataka kuendeleza na kuboresha yale yaliyo asisiwa na mtangulizi wake hasa kwa kutambua kuwa yeye ndio aliyemshawishi kujiunga na chama hicho.

Kuongeza idadi ya wanawake

Akizungumzia namna ya kuongeza wanawake katika siasa, Bertha anasema lazima kuwepo mkakati maalumu ambao utaongeza idadi ya wanawake kushiriki chaguzi mbalimbali ikiwemo uchaguzi mkuu.

Anasema wanaume wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushiriki katika uongozi wa nafasi za juu kuliko wanawake kutokana na kundi hilo kuaminiwa zaidi.

“Vyama vya siasa nchini vinatakiwa kuwapa usaidizi zaidi wanawake kushiriki kikamilifu katika uchaguzi hasa katika nafasi za juu za uongozi badala ya kuwaacha wenyewe,” anasema huku akifafanua zaidi:

“Pia, sera na sheria zinapaswa kuangaliwa katika kuhakikisha wanawake nao wanakuwapo katika uteuzi wa uongozi wa juu,” anasema.

Bertha anabainisha kuwa Tume ya Uchaguzi inapaswa kuangalia masuala ya jinsia kwa kushirikiana na Msajili wa Vyama vya Siasa ili kuhakikisha wanawake wanaingia kugombea nafasi unapotokea uchaguzi.

Mikakati yake

Anasema moja ya mikakati ya chama hicho ni kuendelea kufanya siasa safi za kistaarabu na kuhakikisha kinakua imara bara na visiwani.

“Nitahakikisha chama changu kinakuwa imara bara na visiwani, pia nitahakikisha chama kinaanza kujenga ofisi za chama kila mkoa, lengo likiwa ni kukiendeleza chama kisonge mbele,” anasema.

Anasema pia ataendeleza na kuyaboresha yale yaliyoasisiwa na mtangulizi wake.

“ Unapokuwa kiongozi, changamoto haziepukiki, kinachotakiwa ni kuzikabili ndio maana tumefanya uchaguzi wa kuchagua viongozi mbalimbali katika chama chetu kwa lengo la kukijenga na kukifanya chama kisonge mbele kwa kusimamisha wagombea makini katika uchaguzi ujao,” anaongeza.

Azungumzia Serikali

Mwenyekiti huyo anaimwagia sifa Serikali. “Naipongeza Serikali ya awamu ya tano katika kulinda rasilimali za nchi ili ziwanufaishe Watanzania, lakini pia isisahau kuchukua ushauri wote wenye maslahi ya kujenga taifa na kulinda amani ya nchi na kamwe wasichukue ushauri wenye nia ya kuhatarisha usalama wa nchi kwani amani tuliyonayo inapaswa kulindwa kwa nguvu zote kwani ndio fahari ya Tanzania,” anasema Bertha.

Mwenyekiti huyo anasema ni muda muafaka kwa Serikali kubadilisha sheria ya vyama vya siasa na kuwepo na kipengele kitakachoweza kutambua juhudi za vyama vya siasa visivyokuwa na uwakilishi bungeni na kuanza kuvipa ruzuku, japo kidogo, ili viweze kujiendesha.

“Ni changamoto kubwa kwa vyama visivyo kuwa na uwakilishi bungeni kuendesha shughuli zake za kila siku,” anasema Bertha

Anafafanua kuwa kwa sasa chama chao kinajiendesha kupitia michango mbalimbali ya viongozi na mauzo ya kadi.

“Chama chetu hakina ruzuku kwa sababu hakikufanikiwa kuwa na diwani wala mbunge katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini mwaka 2015, hivyo nitumie nafasi hii kuiomba Serikali ifikirie sasa vyama visivyokuwa na uwakilishi bungeni iweke utaratibu wa kuvisaidia kwa kutoa ruzuku kwa sababu wote tunafanya kazi moja, tunafanya kazi ya kuielimisha Jamii,” anabainisha.

Chanzo: mwananchi.co.tz