Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki zinavyoshindana kubadilisha fedha maeneo nyeti

Tue, 19 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ukaguzi kisha kufungwa kwa maduka ya kubadilisha fedha kulianza jijini Arusha mwishoni mwa mwaka jana halafu Dar es Salaam mapema mwaka huu hivyo kutoa nafasi kwa benki za biashara kuchangamkia fursa. Sasa zinashinda kweli kweli.

Licha ya huduma hiyo kupatikana kwenye matawi yote ya benki za biashara, ushindani unazidi kuwa mkubwa miongoni mwao kiasi cha kuongeza ubunifu unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

Licha ya ujumbe wa maneno unaotumwa kwenye simu za wateja wa benki husika nchini, baadhi ya taasisi hizo zinatumia mitandao ya kijamii kutangaza huduma zao.

Katika miakati yao, zipo zinazotumia magari maalumu yanayotoa huduma za kibenki pamoja na kubadilisha fedha katika viwanja vikubwa vya ndege kwa mfano Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na ule wa Kilimanjaro (KIA).

Benki za NMB, CRDB na TPB ni miongoni mwa zinazoshindana kwa kusambaza magari hayo hutoa huduma zote muhimu kwa wateja wao kwenye viwanja hivyo.

Mkuu wa idara ya mawasiliano wa Benki ya NMB, Joseline Kamuhanda alisema wamekuwa wakibadilisha fedha tangu siku nyingi lakini kufungwa kwa maduka ya kubadilisha fedha kumeongeza fursa na wamejipanga vyema kuwafikia wateja wengi zaidi kadri iwezekanavyo.

“Kila tawi tumehakikisha kuna dirisha maalumu la kubadilishia fedha na kwenye viwanja vya ndege kuna magari haya maalumu yanayotoa huduma hiyo pia,” alisema Joseline.

Ofis amtendaji mkuu wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi alisema tangu kufungwa kwa maduka, benki za biashara zina jukumu la kuhakikisha huduma inaendelea kupatikana maeneo yote kama ilivyokuwa zamani.

“Tulikuwa wa kwanza kuanza kutoa huduma hii kwenye viwanja vya ndege JNIA,” alisema na kufafanua kuwa wanalo gari maalumu linalowahudumia wageni wanaotembelea nchini.

Mkurugenzi wa huduma mbadala wa Benki ya CRDB, Philip Alfred wateja na wasio wateja wa benki hiyo, Watanzania na wageni vilevile, wanaweza kupata huduma ya kubadilisha fedha kwenye matawi yote ya benki hiyo yaliyopo nchini.

“Lengo ni kuhakikisha tunakidhi mahitaji yaliyopo. Vilevile, tumeimarisha huduma zetu KIA na JNIA kw akuongeza mashine ya kutolea fedha pamoja na gari maalumu,” alisema.

Huduma hizo, alisema zitawarahisishia Watanzania wanaosafiri kwenda nje ya nchi au wageni wanaoingia nchini kwa malengo tofauti ama kununua sarafu za nje au Shilingi ya ndani.

Novemba mwaka jana, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilifanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka ya kubadilishia fedha mkoani Arusha ili kudhibiti ukiukwaji wa sheria, kanuni na utaratibu wa biashara hiyo.

Mwezi mmoja baadaye, Rais John Magufuli alisema kuna ukwepaji kodi miongoni mwa wafanyabiashara waliokuwa kwenye sekta hiyo. Rais alisema wapo ambao walikuwa wanatumia leseni moja kwenye maduka mpaka saba ya kubadilisha fedh akinyume na utaratibu.

 “Katika maduka 37 yaliyokaguliwa, ni moja tu lilikuwa limesajiliwa,” alisema Rais Magufuli.

Mwezi uliopita, BoT ilifanya ukaguzi kama huo jijini Dar es Salaam na ikayafunga zaidi ya maduka 50 yaliyobainika kukiuka utaratibu uliopo.



Chanzo: mwananchi.co.tz