Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki zaombwa kukopesha viwanda vidogo vya sukari

578fad5c83c9fb0c35903f7610b5162d Benki zaombwa kukopesha viwanda vidogo vya sukari

Thu, 4 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imeziomba benki nchini kutoa mikopo kwa kampuni za uwekezaji wa shughuli za kilimo na ujenzi wa viwanda vidogo vya uzalishaji wa sukari, ili kulipunguzia taifa mzigo wa kuagizaji sukari kutoka nje ya nchi.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema hayo alipofanya ziara katika Kiwanda cha Sukari TPC na kufanya kikao cha ndani na menejimenti ya kiwanda hicho sanjari na bodi ya sukari nchini.

"Benki hapa nchini zitoe mikopo kwa wawekezaji katika ujenzi wa viwanda vya sukari hususan vile vidogo vidogo, yupo mwekezaji mmoja pale Mikumi mkoani Morogoro anaitaji mtaji wa Shilingi bilioni kumi tu, benki zetu hazikosi fedha hizi,"alisema.

Alisema iwapo mwekezaji huyo angepata fedha hizo angewekeza na kutoa fursa za ajira, huku ikiwahakikishia wakulima wa miwa kuwa na uhakika wa soko la miwa yao ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.

Hata hivyo Waziri Mkenda amezipongeza benki za CRDB na NBC kwa kutoa mkopo katika kiwanda cha TPC na kukifanya kuwa kiwanda cha mfano Tanzania, Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema mikopo iliyotolewa katika kiwanda cha TPC imefanikisha kuboreshwa kwa mitambo pamoja na shughuli za kilimo jambo ambalo limeongeza tija na hivyo kiwanda hicho kujiendesha kwa mafanikio makubwa.

Waziri Mkenda alisema TPC sasa ina uwezo wa kuzalisha tani 140,000 za miwa kwa hekta, kiwango ambacho ni kizuri sana duniani.

Mapema Ofisa mtendaji utawala wa TPC, Jaffary Ally alisema kiwanda hicho ni cha mfano ambapo wamekuwa na mafanikio makubwa kwa kipindi cha miaka 20 sasa.

Alisema TPC imeongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 za sukari mwaka 2000 wakati kinabinafsishwa hadi tani 110,000 za sukari hadi kufikia mwaka jana.

Ally alisema kwa mwaka huu TPC imezalisha tani 103,000 za sukari na kuvuka malengo ya msimu uliopita wa kuzalisha tani 95,000 ambao ulipata changamoto ya kukumbwa na mafuriko.

Chanzo: www.habarileo.co.tz