Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya wachimba madini yaja

Madini Pic Data Benki ya wachimba madini yaja

Tue, 30 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wachimbaji madini nchini wameazimia kuanzisha benki yao itakayowawezesha kuwapa mitaji ya kuchimba madini kwa tija.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (Femata) John Bina ameyasema hayo jijini Arusha leo Jumanne Mei 30 kwenye kikao cha wachimbaji madini cha kujadili uanzishwaji wa benki hiyo.

Bina amesema uanzishwaji wa benki hiyo utajibu changamoto mbalimbali za wachimbaji na wadau wote wanaonufaika na mnyororo wa thamani ya madini.

Ametaja wanufaika wa benki hiyo ni wachimbaji madini wakiwemo wamiliki wa leseni, wenye mialo, wenye migodi, miduara, wachenjuaji, wanunuzi wa magonga ya Tanzanite, wanunuzi wakubwa wa madini wa kati na wachuuzi.

"Mchakato wa uanzishwaji benki unahitaji maoni, uzoefu na utaalam ili kujiweka tayari hasa kununua hisa pindi benki hiyo ikianza," amesema Bina.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) Dk Venance Mwasse amesema uanzishwaji wa benki hiyo ni maendeleo makubwa na umuhimu hasa kwa wachimbaji wadogo nchini kwani hawana mitaji.

Dk Mwasse amesema wazo la uanzishaji wa benki ni zuri kwani hata mataifa mengine ya nje yataiga kwenu kwani mmetegua mtego mkubwa wa kuwa na benki yenu.

"Mtaona fahari kuwa hata sisi wachimbaji wadogo tunaongeza mtaji wa nchi katika mapato kwa kuwa na benki kwani uchumi mkubwa ulioendelea ni ule uliopo katika mfumo wa benki," amesema Dk Mwasse.

Amesema wachimbaji madini wakikopesheka wataweza na kwamba tasnia ya wachimbaji wadogo isipoendelezwa haitapiga hatua kwani wengi wao wanafanya shughuli hizo kwa sababu ya kujikimu kimaisha.

Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Musukuma (CCM) ambaye amewawakilisha Wabunge wanaotoka kwenye maeneo yenye migodi amesema uanzishwaji wa benki hiyo ni wazo zuri litakuwa kimbilio kwa wachimbaji.

"Nitahakikisha tunamshawishi Rais Samia Suluhu Hassan ili aongoze harambee ya uanzishwaji wa benki hii ya wachimbaji wa madini," amesema Musukuma.

Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Laizer amesema uwepo wa benki hiyo itakuwa fursa kubwa kwa wachimbaji wadogo wengi wasio na mitaji ya kuchimba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live