Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya Standard yatetea bomba la mafuta

Bomba La Mafuta TANGA Benki ya Standard yatetea bomba la mafuta

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: mwanachidigital

Standard Bank Group, benki ya kimataifa na yenye ushawishi katika ufadhili wa miradi mikubwa ya maendeleo barani Afrika imesema ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) utakuwa na manufaa kwa wakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Standard Bank Group kanda ya Afrika Mashariki, Patrick Mweheire alinukuliwa na shirika la habari la Bloomberg akisema miradi hiyo itakuwa na manufaa kwa mataifa yote mawili; Tanzania na Uganda.

Katika ufafanuzi wake, Mweheire alisema utekelezaji wa mradi huo utapunguza athari za ukataji miti.

“Mojawapo ya masuala makubwa nchini Uganda ni kwamba asilimia 70 ya n ishati ya kupikia bado hufanywa kwa mkaa na kuni hivyo wanakata sana miti,” alisema.

Mweheire ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku 12 tangu Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) lizitake nchi husika kuusitisha mradi huo kwa madai ya kutozingatia viwango vya kimataifa vya tahadhari za mabadiliko ya tabianchi huku likichochea ushawishi kwa wadau wengine kuususa.

Mradi huo wenye thamani ya dola 3.5 bilioni utakuwa na urefu wa kilomita 1,445 asilimia 80 zikiwa upande wa Tanzania ukihusisha ubia wa asilimia 62 wa kampuni ya Total ya Ufaransa.

Licha ya azimio hilo kutokuwa na nguvu kisheria, kuna ushawishi wa wanaharakati, taasisi za fedha zinazoshinikiza Total Energies ijiondoe katika uwekezaji huo kutokana na ukiukwaji wa haki za mazingira na haki za binadamu. Wanaharakati hao waliandamana mbele ya Bunge la Umoja wa Ulaya Oktoba 10.

Bunge la Ulaya limemwita Mtendaji Mkuu wa Total Energies, Patrick Pouyanné huku Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akisema atakuwa tayari kutafuta mwekezaji mwingine endapo Total itajiondoa.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakidai kuwa utekelezaji wa mradi huo utaathiri mazingira ikiwamo kuongeza kina cha bahari, kuharibu chanzo cha Ziwa Victoria, bonde la Mto Nile na kuzalisha zaidi ya tani milioni 37 za hewa ya ukaa kwa mwaka.

Hata hivyo, mradi huo unajibu hoja hiyo kwa kutumia Mpango wa Kulinda Mazingira na Usimamizi wa EACOP, Tathmini ya Mazingira na Athari za Kijamii (ESIA) uliothibitishwa Novemba 2019 pamoja na Mpango wa Utayari katika Kulinda Haki za Binadamu wa kulinda na kuhifadhi mazingira.

Tayari Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alishatoa msimamo wa Afrika kuheshimiwa katika utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Nishati, Januari Makamba wakieleza namna mradi huo ulivyoyazingatia mazingira.

Mbali na kauli hizo, Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira Uganda (NEEMA) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zilipinga msimamo wa Bunge hilo

Vita hivyo vya kimazingira vilimgusa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), Dk Peter Mathuki aliyeweka wazi kupitia ukarasa wake wa twitter, akisema “mradi unatoa majibu ya changamoto za muda mrefu katika ukanda huu. Manufaa ya kiuchumi kwa watu wetu, EAC tunajali watu na mazingira.”

Kampuni ya EACOP wiki iliyopita kupitia tovuti yake iliweka wazi kuhusu fidia kwa walioathiriwa na mradi ikiwa ni miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na Bunge la Ulaya likilaani hujuma kwa waathirika hao.

Katika ufafanuzi wake, ilinukuu kwamba wakati ujenzi ukitarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu, ni 331 tu kati ya 9,513 waathirika na mradi huo nchini Tanzania ambao watahamishiwa katika makazi mengine na ujenzi wa nyumba hizi unaendelea.

“Kwa Uganda, kati ya kaya 3,648 ni 203 ndizo zitalazimika kuyahama makazi yao, na wengi wao wamechagua makazi mbadala. Hizi pia ziko chini ya ujenzi,” inasomeka taarifa hiyo.

Chanzo: mwanachidigital