Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya Posta yatoa gawio la Sh1 bilioni kwa Serikali ya Tanzania

66172 Pic+gawio

Wed, 10 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali ya Tanzania imepokea gawio la Sh1 bilioni kutoka Benki ya Posta Tanzania (TPB) linalotokana na faida ya uwekezaji wake wa asilimia 83 ya hisa  katika Benki hiyo katika mwaka wa fedha 2018/19.

Hafla ya makabidhiano ya Hundi kifani ya gawio hilo imefanyika jana Jumanne Julai 9, 2019 jijini Dodoma, kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango  ambaye alipokea kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo, Dk Edmund Mndolwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mpango aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali na kuahidi fedha hizo zitatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

“Utoaji huu wa gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki inazidi kukua na kuwapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa TPB inatoa huduma bora katika jamii,” alisema Dk Mpango.

Pia, aliitaka Benki hiyo kuongeza wigo wa utoaji huduma ili kuwafikia wananchi hususani waishio vijijini pamoja na kutoa elimu kwa wananchi hao kuhusu umuhimu wa  kuweka akiba, kukopa sambamba na kurejesha mikopo kwa wakati.

“Riba katika benki zetu bado ni kubwa taasisi za fedha zione namna ya kuzipunguza sambamba na kutoa mikopo kwa kuzingatia kanzidata ya wakopaji ili kuepuka mikopo chechefu,” alisisitiza Dk Mpango.

Pia Soma

Dk Mpango pia aliiagiza Benki hiyo kuendelea kuwapa wanawake  kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za fedha na mikopo ili waweze kuendesha shughuli za maendeleo, huku pia akiitaka kusimamia uadilifu kwa watumishi wake na kuwa makini na kutoa taarifa za  miamala yenye mashaka ili kuzuia utakasishaji wa fedha haramu.

Naye Dk Mndolwa alisema gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh17.2 bilioni kabla ya kodi ambayo Benki yake imeipata katika mwaka wa fedha 2018/19.

Mbali na kuipongeza Serikali kwa utendaji mzuri ambao umeiwezesha Benki hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, aliahidi kuendelea kushirikiana nayo ili kukuza uchumi wa nchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz