Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya NMB imeshinda tuzo nyingine nne za kimataifa

Image 1 Benki ya NMB yashinda tuzo nne za kimataifa

Fri, 17 Sep 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya NMB imeshinda tuzo nne za kimataifa zote zikiitaja kuwa Benki bora zaidi Tanzania.

Kwa mwaka 2021 NMB imepokea jumla tuzo sita za Kimatifa hivyo kudhihirisha ubora na upekee wa huduma zake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema tuzo hizo ni matokeo ya benki hiyo kuwa rafiki kwa wateja wake.

Tuzo hizo ni pamoja na Tuzo ya Benki Bora ya Biashara na Benki Bora ya Huduma za Uwekezaji Tanzania mwaka 2021 zote kutoka Jarida la World Economic Magazine, Tuzo ya Benki Bora kwa Ubunifu wa Huduma za Wateja Binafsi kutoka Jarida la International Banker na Tuzo ya Benki Bora ya Wateja Binafsi kutoka Jarida la International Business.

Itakumbukwa mapema mwaka huu, Benki ya NMB ilitajwa kwa mara ya tisa mfululizo kuwa Benki Bora zaidi Tanzania na Jarida la kimataifa la Euromoney na Benki Bora ya wateja Binafsi kutoka Jarida la Global Banking and Finance.

"Hizi ni tuzo za juu kabisa za ubora zinazotolewa na majarida makubwa duniani yenye makao yake makuu jijini London na nchini Marekani," amesema Zaipuna.

Amesema kuwa tuzo hizo zimetolewa kwa kuzingatia vigezo kadhaa kwa benki vilivyopendekezwa vya ufanisi wa mahesabu na utendaji kwa ujumla, mkakati wa huduma za kidijitali, huduma jumuishi za fedha, usalama wa huduma za kimtandao na uwajibikaji wa benki katika jamii inayoizunguka.

"Leo hii, zaidi ya asilimia 93 ya miamala yote ya benki ya NMB inafanyika nje ya matawi ya benki.Vigezo vingine vilivyotumika ni mtaji wa benki, mapato yatokanayo na mali za kampuni, uwiano wa fedha na gharama za uendeshaji, kiwango cha amana za wateja, Kiwango cha Mikopo katika soko, Uwiano kati ya mikopo na amana za wateja, uwiano wa mikopo isiyolipika, na uwiano wa hasara itokanayo na mikopo isiyolipika," amesema na kuongeza kuwa;



“Tuzo hizi zinadhihirisha nafasi ya uongozi wa Benki ya NMB katika sekta ya kibenki nchini. Jopo la majaji wa tuzo zote nne waliona kuwa huduma za kidigitali, suluhisho katika huduma za uwekezaji, pamoja na mchango wa benki katika jamii, zimechangia katika ushindi huo

“Benki imeendelea kuboresha huduma zake ili kufikia mahitaji ya wateja, hivyo kuziba pengo la huduma na suluhishi za kifedha sokoni.”

 “Ni mafanikio makubwa kwa Benki ya NMB kupata tuzo sita mwaka huu. Tunajivunia kuwa juhudi zetu zinatambuliwa na hatutaacha kuwa wabunifu zaidi, tunatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kufikia viwango vya juu duniani na mwisho kuendeleza dira yetu ya kuwa benki inayoongoza na benki bora zaidi Tanzania.” amesema Zaipuna



NMB imeendelea kuleta matokeo chanya kwa jamii za kitanzania kwa kuleta huduma zenye ubunifu wa hali ya juu na kuiweka jamii karibu zaidi kwa Benki hususan baada ya uzinduzi wa asasi ya kiraia ya NMB Foundation na Mpango wa Ufadhili wa masomo wa Nuru Yangu Scholarship and Mentorship Program kwa watoto  wenye ufaulu wa juu kutoka kaya masikini.
Chanzo: www.tanzaniaweb.live