Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya NBC yazindua njia mpya ya kukutanisha wafanyabiashara

Benki ya NBC yazindua njia mpya ya kukutanisha wafanyabiashara

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Juhudi binafsi za wafanyabiashara kwa kushirikiana na taasisi za kifedha ni moja ya nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya mpango mkakati wa serikali ya awamu ya tano kufikia  uchumi wa viwanda.

Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Bodi ya benki ya NBC,  Dk Kassim Hussein katika hafla ya uzinduzi wa klabu ya biashara ya benki hiyo , maarufu kama ‘NBC B-Club’ ya Mkoa wa Morogoro ikiwa ni klabu ya 11 kuzinduliwa katika mikoa mbalimbali nchini .

Amesema klabu hiyo  itakuwa faida kubwa kwa wafanyabiashara na nguvu ya kuleta maendeleo kwa taasisi na mtu mmoja mmoja, huku benki  NBC ikiongeza mafunzo ya mara kwa mara kwa kuleta wataalam mbalimbali na kutoa punguzo la riba kwa wanachama wa klabu hizo.

“Kwenye biashara serikali imefanya mageuzi makubwa mfano  katika kuwahamasisha wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki, kurasimishwa kwa biashara, lakini kunahitaji juhudi kubwa katika kuangalia masuala ya masoko, vifungashio, mitaji na viwango vya  TFDA ili kufanya biashara hizo zikue”, amesema.

Akizungumza kuhusu klabu hiyo Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara NBC, Elvis Ndunguru, amesema lengo ni kuwakutanisha wafanyabiashara ili kuweza kubadilishana uzoefu, kupata fursa mbalimbali za masoko ndani na nje ya nchi pamoja na kuwaunganisha na wafanyabiashara wa nje.

Amesema kupitia klabu hizo ni rahisi kutoa nafasi ya elimu kwa wafanyabiashara hao kupitia klabu zao, kwenye maeneo wanayobaini yanayotakiwa elimu baada ya kupata mrejesho toka kwa wateja wao.

“Klabu za Biashara tumeshazianzisha maeneo mbalimbali Tanzania, lakini lengo hasa ni kuwakutanisha wafanyabiashara mbalimbali ili kuweza kugundua fursa, kuwapa  elimu, kuleta wataalam tofauti, pia kuna fursa za kupeleka wafanyabiashara katika nchi mbalimbali” amesema Ndunguru.

Amesema  wanatarajia kuongeza nchi nyingine ambazo zinafanya vizuri kibiashara ikiwemo Uturuki,  Ujerumani na Marekani huku akibainisha kuwa  wana mpango wa kutengeneza dirisha maalum la wafanyabiashara wanawake wadogo na wakati ili kuwahamasisha zaidi kuingia katika biashara.

Akizungumza kwa  niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Ofisa Uvuvi na Mifugo Manispaa ya Morogoro, Mohamed Chamzimu, amesema klabu hiyo itawawezesha wanachama hao kuwa na uelewa wa biashara wa kisasa, na kwamba mafunzo wanayoyapata yataleta tija na kuongeza weledi katika shughuli zao.

Kwa upande wao wafanyabiashara hao akiwemo Bupe Kamugisha wameipongeza benki hiyo kwa huduma bora na masharti nafuu ya kuchukua mikopo, na kusema kwamba imekuwa haina vitendo vya kutaifisha mali za wateja wao pindi wanapopata ugumu kwenye marejesho.

Lusako Mwakiluma amesema mafunzo waliyoyapata  toka kwa taasisi mbalimbali zikiwemo Taasisi ya Kusaidia Sekta Binafsi ya Kilimo (PASS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) yatawasaidia kuboresha biashara zao sambamba na kujua utaratibu unaowapasa kufuata ili kuweza kukidhi viwango vinavyotakiwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz