Kwa mara ya kwanza nchini, wakulima wa zao la tumbaku mkoani Tabora wamelipwa fidia na Benki ya NBC kufuatia hasara waliyoipata kutokana na uharibifu wa mazao yao baada ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika msimu uliopita.
Fidia hivyo imelipwa kupitia mpango wa Bima za Mazao wa Benki ya NBC. Katika mpango huo, Vyama vinne vya Ushirika (AMCOS) vya Insolelansabo, Muloku, Ngulu Moja na Isenegezya vimepewa zaidi ya shilingi milioni tisa, kufidia hasara iliyosababishwa na kuwepo kwa kiwango cha juu cha mvua na hivyo kuharibu mazao na kusababisha hasara kwa wakulima hao.
Akizungumzwa wakati wa kukabidhi hundi ya fidia kwa vyama hivyo, Mkurugenzi wa Wateja wadogo wa Benki ya NBC, Elibariki Masuke alisema fidia hiyo imetolewa kupitia mpango wa bima kwa wakulima ambayo inawalinda dhidi ya hasara zinazosababishwa na athari za hali ya hewa kama vile ukame, vimbunga, wadudu,mvua ya mawe na mengineyo.
“Kwa msimu wa mwaka huu kupitia vyama ambavyo vilikopeshwa na Benki ya NBC katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Shinyanga, wakulima waliweza kupata bima ya Kilimo ambayo iliwawezesha kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali,” alisema.
Alisema hatua hiyo imetokana na upembuzi wa hali ya hewa uliofanyika na kuonekana kuwa katika vijiji vya Lolangulu, Ishishimulwa, Imalakaseko na Isenegzya kulikuwa na kiwango cha juu cha mvua.
Bima hiyo inatolewa na Benki ya NBC kwa kushirikiana na Kampuni ya Bima ya Jubilee. Benki ya NBC inaamini kuwa kupitia bima hiyo, vyama vitapunguza kwa kiwango kikubwa hasara zinazoweza kutokea kutokana mabadiliko ya hali ya hewa na majanga mengine yasiyotabirika na yaliyo nje ya uwezo wa mkulima.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeunda mpango maalum wa kuboresha kilimo ujulikanao kama “ajenda 10/30” ambao unalenga kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilia 5 mpaka 10 ifikapo mwaka 2030, kujitosheleza kwa chakula na kuwawezesha wakulima kubadili uzalishaji wa mazao ya chakula kuwa ya biashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk.Batilda Buriani aliipongeza Benki ya NBC kwa kubuni huduma hiyo ambayo imetoa suluhisho juu ya majanga ambayo yamekuwa yakiwakumba wakulima kwa muda mrefu.
“Naipongeza sana Benki ya NBC kwa kuleta sokoni Bima hii ya mazao yenye lengo la kuwalinda wakulima pindi watapatapo majanga yanayoleta uharibifu wa mazao yao na hivyo kuwaletea hasara.
Hakika bima hii ya kilimo itakuwa ni chachu kwa wakulima wetu wa zao la Tumbaku na wakulima wote nchini, kuweza kulima bila kuwa na hofu juu ya majanga yeyote, tunawashukuru sana Benki ya NBC kwa kuunga mkono adhma ya serikali yetu kwa kuja na huduma hii muhimu sana kwa wakulima wetu.
Nawasihi sasa muongeze bima hii katika mazao mengine ya biashara na chakula ili kutoa ahueni kwa wakulima ambao ndio sekta kubwa na uti wa mgongo wa taifa letu”alisema.