Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya Exim yazindua tawi jipya Mtwara

Kanali Erger Benki ya Exim yazindua tawi jipya Mtwara

Tue, 17 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amewaomba wafanyabiashara mkoani humo kuchangamkia fursa za kibiashara baina ya mkoa huo na nchi jirani ikiwemo Comoro huku akiipongeza Benki ya Exim Tanzania kwa kuwa mstari mbele katika kufanikisha huduma za kifedha baina ya Tanzania na visiwa hivyo.

Akizungumza mapema hii jana wakati hafla fupi ya uzinduzi wa tawi jipya la benki ya Exim mkoani Mtwara lililohamishiwa katika jengo la Sokoine House (PSSF) katikati ya Manispaa ya Mtwara, Kanali Abbas amesema licha ya uwepo wa fursa za biashara kutokana na mahitaji ya bidhaa za chakula ikiwemo maharage, nyama, ulezi na ufuta nchini Comoro changamoto ilibaki kuwa ni huduma za kifedha baina ya mataifa hayo mawili.

Amesema jitihada za benki ya Exim kuboresha huduma hizo utatatua changamoto hiyo.

“Nimefurahi kusikia kwamba benki ya Exim ina matawi zaidi ya matano nchini Comoro na ndio benki inayoongoza kwa ukubwa nchini Comoro na leo hii tunazindua tawi lao jipya na la kisasa zaidi hapa Mtwara.

Jitihada hizi za Exim ndio zinanipa nguvu ya kuwashawishi zaidi wafanyabiashara mkaoni Mtwara na maeneo jirani kutumia vema fursa hii kwa kuwa uhakika wa huduma za kifedha sasa upo…tunawashukuru sana benki ya Exim.’’ amesema.

Kwa mujibu wa Kanali Abbas uzinduzi wa tawi hilo umekuja wakati muafaka kipindi ambacho mkoa huo unatarajia ugeni wa viongozi wakubwa kutoka nchini Comoro watakaoambatana na idadi kubwa ya wafanyabiashara kutoka nchini humo ili kuja kujionea fursa za biashara baina ya mataifa haya mawili.

Awali akizungumza kwenye ya hafla hiyo Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Wateja wa Benki ya Exim, Agnes Kaganda amesema uamuzi wa kuboresha zaidi tawi hilo unalenga kuunga mkono jitihaza za serikali za kukuza uchumi wa mkoa huo kupitia uwekezaji mkubwa kwenye upanuzi wa huduma za bandari na kuboresha hali ya kilimo hatua ambayo inachochea ukuaji wa biashara ya ndani na ile ya kimataifa hususani kati ya Tanzania na Comoro.

“Baada ya kuona jitihada hizo za serikali na kwa kuheshimu wateja wetu tukaona ni vema tuwafungulie tawi lenye hadhi wanayostahili. Tawi hili pia linaendana na mabadiliko makubwa ya huduma za kisasa za kibenki zinazohusisha matumizi ya teknolojia ya hali ya juu katika utoaji wa huduma za kifedha.’’ amesema.

Kwa mujibu wa Kaganda benki hiyo tayari imejipanga kuwahudumia wateja wake wakiwemo wafanyabiashara baina ya Tanzania na Comoro ambapo hivi karibuni ilizindua rasmi huduma yake mpya ya kibenki isiyo na mipaka kati ya mataifa hayo mawili ikilenga kutoa miamala ya gharama nafuu kwa wateja na wafanyabiashara hao.

“Kupitia huduma hii isiyo na mipaka, raia wa Comoro anayetembelea Tanzania kwa sababu za biashara, matibabu au madhumuni yoyote anaweza kutoa fedha au kufanya malipo ya huduma hizo wakati wowote akiwa hapa nchini bila kuathiriwa na sababu za kimipaka baina ya mataifa haya mawili.’’

"Wanachohitaji wateja ni kutembelea matawi yetu mahususi kwa ajili ya huduma hii yaliyopo Dar es Salaam, Zanzibar na hili la hapa Mtwara na hivyo kuwarahisishia kufanya biashara na kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari na usumbufu wa kufanya biashara kwa fedha taslimu,'' amebainisha.

Akizungumza kwa niaba ya wateja wengine wa benki hiyo mkoani Mtwara, Henry Shimo pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa huduma nzuri na heshima inayoendelea kuitoa kwa wateja wake mkoani humo, ameiomba iendelee kuboresha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu zaidi kwa wakazi wa mkoa huo wanaotegemea kilimo, uvuvi na biashara ili waweze kunufaika zaidi na jiografia ya mkoa huo unaopakana na mataifa ya Msumbiji na Comoro.

Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuliwa na wadau mbalimbali wa benki hiyo mkoani humo wakiwemo viongozi wa serikali na wateja wa benki hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live