Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya Exim yatoa msaada wa madawati 100 Tabora

Madawati Msaada Benki ya Exim yatoa msaada wa madawati 100 Tabora

Wed, 13 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya Exim Tanzania imekabidhi msaada wa madawati 100 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 mkoani Tabora ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo wa kutoa msaada wa madawati 1000 katika mikoa mbalimbali hapa nchini ili kuchangia utoaji wa elimu bora kupitia mpango wake wa uwajibikaji wa Jamii (CSR) ujulikanao kama Exim Cares.

Madawati hayo yalikabidhiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mikopo Benki ya Exim Bi Zainabu Nungu kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Buriani wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa huyo Mkoa mapema hii leo.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wengine waandamizi wa Mkoa huo akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda, Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Ndg Solomon Kasaba, Afisa Elimu Mkoa wa Tabora Ndg Juma Kaponda, Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Tabora Ndg Nyahori Mahumbwe, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Tabora Ndg Joel Mkuchika na wadau wengine wa elimu.

Akizungumza mara tu baada ya kupokea msaada huo Balozi Buriani pamoja na kuishukuru benki ya Exim kwa kutoa msaada huo, alisema msaada huo unakwenda sambamba na jitihada za serikali za kuboresha hali ya elimu mkoani humo na kwamba msaada huo utasaidia kupunguza uhitaji wa madawati uliotokana na miradi mingi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa mkoani humo.

“Msaada huu utasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati katika baadhi ya shule zetu…tunashukuru sana wenzetu wa Benki ya Exim kwa msaada huu na tunaomba muendelee kusaidia kwenye maeneo mengine pia ikiwemo sekta ya afya. Mheshimiwa Rais anapambana kutafuta fedha kwa ajili ya miradi mikubwa inayoendelea nchini hivyo ni jambo linalotia moyo kwake kuona wadau kama mabenki mkiendelea kumuunga mkono ” Alisema.

Aidha Balozi Buriani alizitaja baadhi ya shule zitakazonifaika na msaada huo kuwa ni baadhi ya shule zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ambazo zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa madawati.

Kwa upande wake Bi Zainabu Nungu alisema kuwa benki hiyo imejitolea kusaidia katika kuboresha ustawi wa jamii kupitia misaada ya kijamii ikiwemo elimu na kwamba wameguswa sana na suala la changamoto ya madawati kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini, sababu iliyosababisha wao kuchukua hatua hiyo ili kuboresha zaidi sekta hiyo muhimu.

“Ni furaha kwetu kuwa sehemu ya kutatua changamoto kwenye sekta muhimu kama hii. Huu ni mwendelezo tu bado tunaendelea na mikoa mingine kwa kuwa lengo ni kutoa msaada wa madawati 1000 kama tulivyoahidi wakati tunazindua mpango huu mwishoni mwa mwaka jana,’’ alisema Bi Zainabu Nungu huku akiitaja mikoa mingine ambayo imekwisha nufaika na mpango huo kuwa ni Dodoma, Mwanza, Lindi, Shinyanga na Mwanza

Alishauri pia wanafunzi na walimu watakaonufaika na msaada huo kutunza madawati hayo ili yaweze kutumika kwa muda mrefu na hivyo kusaidia walengwa wengi zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live