Benki ya Exim Tanzania jana iliadhimisha miaka 26 ya kuwa zaidi ya benki na kusisitiza tena dhamira yake ya kuendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akizungumza wakati wa hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu, alisema katika kipindi chote cha miaka 26 ya kuwepo kwa benki hiyo, benki hiyo imekuwa mshirika wa kutegemewa na kuchangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.
“Katika kipindi cha miaka 26 iliyopita, Benki ya Exim Tanzania imebadilika na kuwa mshirika wa kutegemewa kwa wateja wetu, na kutoa huduma mbalimbali zinazoendana na mahitaji yao ya kipekee. Kwa sasa, tumeweza kuvuka mipaka ya benki ili kuwa chachu ya ukuaji, ubunifu na maendeleo ndani ya taifa letu,” alisema.
Matundu alisema benki hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa kuzingatia maadili ya uadilifu, uaminifu na umakini misingi ambayo imesaidia kupata uaminifu kwa wateja wake.
"Tunatambua wajibu tulionao katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania na kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara," aliongeza.
Matundu alibainisha kuwa benki hiyo imekuwa ikiwekeza katika miradi inayokuza ujasiriamali, kusaidia maendeleo endelevu na kukuza ujuzi wa masuala ya fedha.
"Tumejitolea kuinua jamii na tumefanya juhudi nyingi kuchangia maendeleo ya Tanzania kupitia programu zetu za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika sekta muhimu zikiwemo elimu na afya, na utunzaji wa mazingira. Kwa kufanya hivyo, sio tu kwamba tumetimiza wajibu wetu kama benki lakini tumekuwa mawakala wa mabadiliko chanya ndani ya jamii zetu,” alisisitiza.
Alisema benki yake imeonyesha dhamira isiyoyumba katika maendeleo ya teknolojia kwa kukumbatia ubunifu wa kidijitali ili kutoa masuluhisho ya kibenki yanayofaa na salama kwa wateja wake.
Mkuu wa Kitengo cha Raslimali Watu Fredrick Kanga wakati wa hafla hiyo alisema benki hiyo iliyoanza na wafanyakazi 15 pekee katika Tawi lake la Samora jijini Dar es Salaam mwaka 1997 leo inaongeza idadi ya watumishi kufikia 600 nchini Tanzania na zaidi ya wafanyakazi 400 katika matawi yake yaliyopo nje ya Tanzania.
"Kama benki, tunaamini kuwa mtaji wetu mkuu ni watu wetu. Tunafurahi kwamba tunaadhimisha miaka 26 ya kuwa zaidi ya benki nah isingetokea bila ueledi wa wafanyakazi wetu. Kuna benki ambazo hazijaweza kudumu kwa muda huu lakini sisi tunaendelea kukua mwaka hadi mwaka,” alisema.