Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya Dunia yaipa Tanzania Sh1.8 trilioni

16196 Pic+wb TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB)imeipatia Tanzania mkopo wa Sh1.8 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi endelevu ya usambazaji maji vijijini na usafi wa mazingira katika wilaya 86 nchini.

Pia fedha hizo zitatumika  kuendeleza uunganishaji wa umeme kutoka Zambia katika mikoa minne ya kusini  mwa Tanzania.

Katika fedha hizo Sh1.04 trilioni  zimetengwa kwa ajili ya usambazaji wa umeme huku Sh800 bilioni ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira.

 Akizungumza leo Septemba 7  katika hafla ya utiaji wa saini kati ya Benki ya Dunia na Tanzania, Katibu mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema mkopo huo wenye masharti nafuu utasaidia katika kupunguza tatizo la maji kwa wananchi na kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia watu wengi zaidi.

"Ni jukumu letu kama serikai kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na kuwa katika mazingira rafiki lakini kwa upande wa vijijini bado ni changamoto kubwa hivyo ni lazima tuhakikishe tunawafikia kupitia vyanzo vya ndani au mikopo," amesema James

Kwa upande wa umeme, James amesema mkopo huo utaisaidia Taasisi katika kuongeza uzalishaji wa umeme na upanuzi wa Miundombinu ya kusafirishia umeme.

"Njia ya usafirishaji umeme kati ya Iringa, Kisada, Mbeya, Tunduma na Sumbawanga utakuwa na uwezo wa 400-kV, Vituo vidogo vya uzalishaji kati ya Sumbawanga, Tunduma, Kisada, Mbeya vitakuwa na 400kV huku ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme kutoka Tunduma hadi Mpaka wa Zambia ukiwa na 330kv," amesema James.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird amesema licha ya kuwa Tanzania inakabiliwa na uchafu wa mazingira unaosababisha magonjwa kama kipindupindu lakini bado watanzania wanaonekana kuendelea kuboresha nyumba zao kuliko vyoo.

"Tunapaswa kuwaambia na kuzihamasisha kaya kuhama kutoka matumizi ya vyoo visivyokuwa safi na salama kwenda katika vyoo safi na salama ili wawe na afya njema itakayowaruhusu kufanya kazi kwa bidii," amesema Bella.

Chanzo: mwananchi.co.tz