Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya Dunia kuwajengea uwezo wajasiriamali wa mafuta, gesi

8842 Pic+benk TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati utekelezaji wa miradi mikubwa ya mafuta na gesi ikiendelea nchini, Benki ya Dunia (WB) imejitoa kuwasaidia wazawa kunufaika nayo.

Miradi hiyo ni pamoja na bomba la mafuta litokalo nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na ule wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG) mkoani Lindi.

Makamu mwenyekiti wa umoja wa watoa huduma za mafuta na gesi nchini (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim alisema mwakilishi mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird amekubali kuusaidia umoja huo kuwajengea uwezo Watanzania wanaotoa huduma za mafuta na gesi ili wasipitwe na fursa zilizopo katika miradi hiyo.

Benki hiyo imeahidi kutoa fedha kwa ajili ya mafunzo ya kukuza uelewa, kuboresha mifumo ya huduma na kuwapa wataalamu wa kuwashauri katika mambo mbalimbali ndani ya sekta.

Muasisi wa ATOGS, Kenneth Mutaonga alisema benki hiyo imewahakikishia kuwasaidia wadau wa sekta hiyo kwa kuwa kufanya hivyo kutakuza uchumi nchini.

“Tulikutana mara ya kwanza Mei 10 na kufanya vikao vya mara kwa mara. Siku nyingine walitukutanisha na mabalozi wa nchi ambazo kampuni zao zinatoa huduma za mafuta na gesi nchini ili kubadilishana uzoefu,” alisema Mutaonga.

Aliongeza kuwa fursa zipo nyingi na Watanzania wana uwezo wa kutoa baadhi ya huduma, tatizo ni mifumo ya kuwatambua licha ya kuwa sheria inaelekeza kuwa katika huduma nyingi kipaumbele kitolewe kwa wazawa.

Chanzo: mwananchi.co.tz