Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki, wakandarasi waoneshwa fursa DRC

55655afb70fb6f77b30f93b1cffe40b2.jpeg Benki, wakandarasi waoneshwa fursa DRC

Tue, 12 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wasomi na wachambuzi nchini wamefichua fursa ambazo wakandarasi, mabenki na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) watazipata baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) huku taifa hilo likioneshwa fursa zake katika kanda.

Wameshauri Wakongo waliopo nchini katika sekta mbalimbali zikiwamo za michezo na burudani, kutumika kulitangaza taifa kuhusu vivutio vya uwekezaji vilivyopo Tanzania likiwamo suala la amani, usalama na demokrasia.

Akizungumza na HabariLEO jana, Mchambuzi wa Masuala ya Diplomasia na Uchumi, Abbas Mwalimu, alisema kutokana na DRC kuzalisha madini mengi yakiwamo ya dhahabu, fedha nyingi zinazotokana na mauzo ya madini hayo zimekuwa zikiwekwa katika benki za mataifa ya Ulaya.

“Hii ni fursa kwetu Tanzania kwa benki zetu kama Benki ya NMB, CRDB na NBC kuwekeza nchini DRC ili kupata biashara kubwa kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa wa madini ambao wanatafuta mahali salama pa kuhifadhia fedha zao,” alisema Mwalimu. Kuhusu TPA, alisema ujio wa DRC katika EAC unaleta fursa kwa mamlaka hiyo kuongeza uwepo wake hususani kwa kufungua ofisi kubwa zaidi nchini humo.

“Ili kulikamata soko lote la Congo, ni lazima TPA iangalie uwezekano wa kupanua shughuli zake ndani ya Congo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwalimu, Tanzania inaweza kupata fursa ya kuwa na soko kubwa la madini kuliko hali ilivyo sasa endapo serikali itafanya uboreshaji mkubwa wa soko hilo kwa ajili ya kuvutia madini ya dhahabu kutoka katika taifa hilo ambalo ni mwanachama mpya wa EAC. Alifafanua kuwa kutokana na ukubwa wa Congo, Tanzania inapaswa kuangalia uwezekano wa kufungua ubalozi katika miji mitatu ya Kinshasa, Goma na Lubumbashi na kuweka utaratibu kwa mabalozi kuwashawishi kupitia vikao wawekezaji na wafanyabiashara wa DRC kuwekeza Tanzania katika nyanja mbalimbali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye pia ni mtaalamu wa Diplomasia na Uchumi, Profesa Humphrey Moshi alisema kutokana na miundombinu ya DRC hususani barabara kutokuwa nzuri, ni fursa kwa wakandarasi wa Tanzania kutumia nafasi hiyo kupata kandarasi nchini humo.

“Mbali na barabara, DRC ina milima na mabonde pamoja na mito mingi inayohitaji madaraja mengi ili kuunganisha maeneo mengi ya makazi ya watu na huduma mbalimbali kama hospitali, shule na masoko...” alisema Profesa Moshi.

Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi na Diplomasia, Profesa Kitojo Wetengere alisema kutokana na wingi wa watu; takriban milioni 90 wa DRC, Tanzania inatakiwa kufanya utafiti ili kujua bidhaa zinazohitajika zaidi nchini humo ili kuzisafirisha na kujipatia soko la uhakika ndani ya kanda. Kuhusu fursa inazoweza kupata DRC kujiunga na EAC, alisema matatizo ya nchi hiyo yanakwenda kumalizwa kwa sababu ni rahisi jumuiya kushughulikia matatizo hayo kwa umoja kuliko nchi mojamoja.

Kuhusu suala hili, Mwalimu alisema DRC itafaidika zaidi na EAC kwa kuwa sasa nchi zinazoguswa na matatizo ya DRC zitakuwa saba na hivyo, kuwa rahisi kutunga sera kwa kila nchi juu ya namna ya kukabiliana na matatizo hayo ya DRC.

Profesa Moshi kwa upande wake, alisema ni jambo jema kwa DRC kujiunga na EAC kwani kutasaidia kulinda na kuziweka salama rasilimali zake zilizokuwa zikiporwa na waasi wakishirikiana na mataifa ya kigeni katika ardhi ya Congo.

“Kujiunga kwa Congo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni fursa nzuri kwao kuboresha miundombinu hasa ya barabara kwa sababu kuna kipengele kinamtaka mwanachama wa EAC kujenga barabara ya Afrika Mashariki kwa kiwango cha lami itakayoiunganisha na nchi wanachama,” alisema.

Alisema ujio wa DRC utaifanya EAC kuwa na nguvu katika kushughulikia matatizo ya Congo kuliko hata Umoja wa Afrika (AU).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live