Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki kupeleka elimu ya fedha majumbani

FEDHA WEB Benki kupeleka elimu ya fedha majumbani

Wed, 8 May 2024 Chanzo: Habarileo

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji na kampuni ya SILABU APP inayotoa huduma za masomo ya ziada kwa wanafunzi majumbani na kwa njia ya mtandao.

Makubaliano hayo yanalenga kushirikisha walimu wa taasisi hiyo kufikisha elimu ya fedha na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kwa wanafunzi wao. Hatua hiyo inatajwa kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaongezea wanafunzi hao elimu na uelewa kuhusu masuala ya fedha na umuhimu wa kujiwekea akiba tangu wakiwa wadogo.

Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo Msimamizi wa Huduma za Elimu wa Benki ya NBC, Yoabu Ndanzi alisema ushirikiano huu utatoa fursa kwa benki hiyo kuweza kuwafikia wanafunzi na walimu kwa urahisi zaidi, hatua ambayo itarahisisha suala zima la kuwajengea uelewa wanafunzi hao kuhusu elimu ya fedha sambamba na kutambua huduma za benki hiyo mahususi kwao.

Aliongeza kuwa kupitia mpango huo watoto watawekewa kiasi cha sh elfu 5 kila mwezi kwenye Akaunti zao za Chanua. Fedha hizi zinafadhiliwa na SILABU APP ili kuendeleza ushirikiano na wateja wao ambao ndio wanafunzi kila mwezi.

Akizungumzia ushirikiano huo Mwanzilishi Mwenza wa kampuni ya SILABU, Adam Duma alisema ushirikiano na NBC utahusisha walimu zaidi ya 1000, utatoa fursa pia kwa walimu hao kunufaika na huduma mbalimbali za vipaumbele zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo akaunti ya Mwalimu huku pia kampuni hiyo ikinufaika kupitia matangazo ya huduma zake kupitia majukwaa mbalimbali ya taarifa za benki hiyo.

Chanzo: Habarileo