Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki inayotembea yashangaliwa Dumila

Utepepic Mkuu wa Wilaya Kilosa, Majid Mwanga akizindua huduma ya benki inayotembea

Thu, 24 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi na wafanyabiashara wa Mji Mdogo wa Dumila mkoani Morogoro, wameanza kunufaika na huduma za kifedha baada ya benki ya NMB kuzindua tawi la huduma za benki inayotembea.

Hatua hiyo ni maandalizi ya kujengwa kwa tawi kubwa la benki kwenye mji huo ambao umekuwa na harakati nyingi za kibiashara.

Mbali na kuzindua benki hiyo inayotembea, NMB pia imetoa msaada wa vifaa vya elimu kwa shule ya msingi Kilosa Town na Sekondari ya Lumuma vyenye thamani ya Sh10 milioni ikiwa ni meza 50 na madawati 50.

Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi amesema wananchi wa Dumila wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za kibenki hivyo, tawi hilo litakuwa limemaliza adha hiyo.

Amesema kwa sasa huduma za kifedha zitakuwa zinatolewa kupitia tawi hilo linalotembea wakati mchakato wa ujenzi wa tawi kubwa ukiendelea.

“Dumila ni mji wenye shughuli za kimaendeleo na wananchi wanaendesha biashara mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, madini hivyo, kukosekana kwa huduma za kibenki ni tatizo kubwa. Tumekuja kumaliza tatizo hilo kwa kuzindua tawi hili na tunajipanga kwa makubwa zaidi,” amesema Mlozi.

Kuhusu misaada kwenye shule hizo, Mlozi amesema NMB imekuwa mshirika wa karibu wa Serikali katika maendeleo na kusaidia huduma za kijamii.

Mkazi wa Dumila, Hawa Mohamed amesema sasa wataondokana na adha ya kutembea umbali kufuata huduma za kibenki Turiani ikiwa ni kilometa 50 au kwenda Kilosa na Mvomero.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Abdu Majid Mwanga amesema Dumila imekuwa na kilio cha muda mrefu cha uhitaji wa mabenki hivyo, ufunguzi wa tawi la NMB unakwenda kuondoa changamoto hiyo.

“Siwapigii debe hawa NMB lakini wamekuwa na mikopo ya wafugaji ili kufuga kwa kisasa, pia kuna kilimo na kusaidia huduma za kijamii ikiwemo sekta ya elimu na afya,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live